28 January 2013

Stewart avua nguo Chamazi


Na Mwandishi Wetu

KITENDO cha kocha wa Azam FC, Stewart Hall kuonyesha nguo yake ya ndani, kimetafsiriwa tofauti na mashabiki waliohudhuria mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu  yake ilipoumana na Kagera Sugar, juzi katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.


Stewart alifanya hivyo wakati mchezo huo ukiendelea muda mchache baada ya kulalamikia maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo lakini mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo wakamgeuzia kibao na kuanza kumzomea ndipo alipoamua kushusha bukta yake na kuonyesha nguo yake ya ndani.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Mkoa wa Kagera, Jacob Kilyanga alisema kitendo hicho ni kinyume na maadili kufanywa na kocha hasa katika umati wa watu.

Alisema hatalifumbia macho suala hilo, atalifikisha katika kamati husika kuanzia Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kukemea tukio hilo la udhalilishaji.

"Sio kitu kizuri kwa kocha huyo wa kimataifa, nimeshangazwa na tukio hilo, sikutegemea kama yeye anaweza kufanya, anafundisha kitu gani wachezaji wake na jamii kwa ujumla, nitalifikisha TAFCA na hatua zichukuliwe" alisema Kilyanga.

Kitendo hicho pia kimekerwa na kocha Kenedy Mwaisabula na kutaka kuona TFF inachukua hatua dhidi ya kocha huyo.

Kocha Stewart hii si mara yake ya kwanza kufanya hivyo, amekuwa akifanya hivyo pindi anapoona mashabiki wanaizomea timu yake au kufanyiwa vitendo visivyo vya haki.

No comments:

Post a Comment