03 January 2013
Polisi Mbeya yawaonya askari wake
Na Rashid Mkwinda, Mbeya
JESHI la Polisi mkoani Mbeya, limesema litamfukuza kazi polisi yeyote ambaye atabainika kufanya vitendo vya uhalifu pamoja
na kuwalazimisha raia wampe rushwa.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athumani, aliyasema hayo jana katika mahojiano na waandishi wa habari yaliyorushwa moja kwa moja na Kituo cha Redio cha Bomba FM, mjini humo.
Alisema hatavumilia kuona askari anayetuhumiwa kula rushwa akiendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwa kitendo hicho kinalitia doa Jeshi la Polisi katika uwajibikaji wake.
“Zipo changamoto nyingi katika Jeshi la Polisi, tutajitahidi kurejesha mahusiano na jamii kwa kuwajibika ipasavyo, askari atakayebainika kula rushwa au kufanya kosa lolote la jinai atafukuzwa kazi.
“Tangu niwasili mkoani hapa miezi sita iliyopita, polisi wanne wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ambayo yalikiuka weledi na uwajibikaji wao katika jamii,” alisema.
Akizungumzia suala la askari polisi kuhusika katika ubambikaji wa kesi na kutumia Vituo vya Polisi kama maeneo ya kutolea adhabu kwa kuwashinikiza raia kukiri makosa, Kamanda Athumani alisema watuhumiwa husika wanapaswa kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo.
Katika kukabiliana na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, Kamanda Athuman alisema idadi ya vituo vya askari wa usalama barabarani vimepunguzwa ili kuepuka vitendo vya rushwa.
“Raia wanapaswa kuwa mstari wa mbele na kutoa taarifa za rushwa kwa Jeshi la Polisi juu ya askari wa usalama barabarani, tusaidiane katika hili na kupeana taarifa, huu ndio ushirikishaji wananchi kwenye dhana ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi,” alisema.
Alisema ili kuwaponguzia kazi askari, raia wanapaswa kupima aina ya makosa wanayopeleka kituoni hususan kesi za madai ambazo mahali pake ni mahakamani.
“Kesi za madai tusikimbilie kuzipeleka Kituo cha Polisi, tukazifungue mahakamani, hii itatusaidia kuondoa ushawishi
wa askari polisi kutaka hongo,” alisema.
Awali Kamanda Athumani alisema, kipindi cha Januari hadi Desemba 2012, makosa ya jinai yalikuwa 29,849 ambapo
mwaka 2011, yalikuwa 25,699 hivyo ongezeko ni makosa
4,150 sawa na asilimia 16.
Ongezeko hilo limetokana na makosa ya kutumia lugha za matusi, kutishia, wizi na shambulio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment