29 January 2013

PFT yaitaka jamii kufahamu umuhimu wa VICOBANa Rose Itono

SHIRIKA la Kupambana na Umasikini (PFT) limeitaka jamii kufahamu kuwa VICOBA ni silaa kubwa katika kupambana na umasikini.

Akizungumza Dar es Salaam juzi katika hafla ya uzinduzi wa VICOBA katika kikundi cha Vibukiyo B, Mkurugenzi Mtendaji wa PFT Bw.Issa Mohamed alisema,ili kuweza kukuza uchumi ni wajibu wa jamii kukaa katika vikundi na kubuni miradi ili kuweza kujipatia kipato.

Alisema kuwa,kwa kufanya hivyo kutawezesha jamii kupitia vikundi kupata mikopo ya pamoja na kuweza kupambana na umasikini.

Mkurugenzi alizitaka taasisi zinazojihusisha na utoaji mikopo yakiwemo mabenki mbalimbali yaliyopo nchini kubadilisha sera zao ili ziweze kuendana na matakwa ya wanavikundi.

"Kumekuwa na masharti makubwa katika kupata mikopo hali inayofanya wanavikundi hasa wanawake kushindwa kutumia fursa hizo kupata mikopo',alisema.

Alisema kuwa,mabenki mengi yamekuwa yakitoa masharti magumu ambayo yamewafanya wanavikundi kushindwa kukopa na kusababisha hali ya umasikini kuendelea kuwepo.

"Vikundi hivi vinategemea taasisi za fedha hivyo mkiweka mashati magumu mnawanyima fursa ya kukuza uchumi",alisisitiza.

Hata hivyo Meneja Mwendeshaji Mwandamizi wa Benki wa wanawake Bi. Magreth Msengi aliwataka wanavikundi kuitumia Benki hiyo ili kuweza kukopa na kukuza mitaji yao.

Alisisitiza kuwataka wanavikundi kuwa waaminifu pale wanapopatiwa mikopo ili kuweza kupata fursa za kupata mikopo mikubwa zaidi na kuinua uchumi wao.

Alisema kuna baadhi ya wanavikundi wamekuwa si waaminifu na kusababisha wenzao kupata kazi ya kuwalipia madeni pale wanapowakimbia.

Alisema Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali kwa jamii bila kujali jinsia yeyote kwa faida ya nchi.

No comments:

Post a Comment