03 January 2013
Pengo aguswa na wimbi la watoto mitaani
Na Grace Ndossa
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesikitishwa na wimbi la watoto wa mitaani linaloongezeka kila kukicha duniani.
Alisema mamilioni ya watoto wanateseka kwa kukosa pa kukakaa huku wakilia na kuomboleza lakini hakuna mtu anayewaonesha matumaini hivyo kusababisha wengine kufariki dunia.
Mwadhama Pengo aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika Ibara ya Misa Takatifu ya kuwakumbuka watoto mashahidi waliouawa bila kosa kwa amri ya Mfalme Herode.
Ibada hiyo aliyofanyika katika Viwanja vya Msimbazi Center, kushirikisha watoto kutoka maeneo mbalimbali ya Parokia za
jimbo hilo, walezi wao, mapadri, watawa na waumini wengine.
“Watoto wengi wanalia kilio kisicho na maana mbele ya binadamu wengine na kuteseka hadi kufa, sisi kilio chetu tuweke mbele za Mungu kwa kuwaombea,” alisema Mwadhama Pengo.
Aliongeza kuwa, watoto hao wangepata faraja na matumaini kama jamii itabadilika na kuwahurumia kutokana na mateso mbalimbali wanayokumbana nayo.
Alisema kazi iliyobaki ni kuwaombea kwa Mungu ili kilio chao kisaidie ukombozi wa dunia ya leo kwani Yesu Kristo alipokea mahangaiko ya watoto Yerusalem.
“Kupitia sara zetu, Mungu atakomesha mahangaiko ya watoto
katika dunia ya leo,” alisema na kuongeza kuwa, viongozi ambao wanashindwa kufuata maelekezo ya Mungu, hawezi kufanikiwa katika njia zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment