07 January 2013
Muccadam aongoza wananchi operesheni usafi Jangwani
Na David John
MLEZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Jimbo la Ilala Bw.Kamaldeen Muccadam amewaongoza wakazi wa Bagidadi Mchikini eneo la Jangwani kufanya uperesheni ya kusafisha mitaro kutokana na kujaa kwa uchafu na kusababisha mafuriko.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuona kuwa kuna uwezekano wa kutokea athari kubwa na hasa milipuko ya magonjwa na kusababisha watu kupoteza maisha.
Bw.Mccudam alisema ameamua kutatua kero za wakazi hao wa kata ya Mchikichini na Jangwani kutokana na wakazi hao kuishi kwa muda mrefu katika mzingira hatarishi lakini bado viongozi wa mtaa,kata na Serikali wameshindwa kuwawekea mazingira mazuri ya usafi wa mitaro.
"Nimeguswa katika hili kwani hii ni hatari wananchi hawa wamesahaulika na wamekuwa kama hawana baba wala mama hali na ndio maana nikaguswa kuwasaidia kusafisha mitaro na kukodi greda ambalo lilitumika kusafisha bonde la mto ili maji yaweze kupita kwa urahisi, "alisema Bw.Mccudam.
Aliongeza kuwa sababu nyingine iliyomsukuma kugharamia zoezi hilo baada ya wananchi kumwomba msaada wa fedha kwa ajili ya usafi wa mazingira ikiwa pamoja na kuzibua mitaro iliyoziba.
"Si mara ya kwanza kutoa msaada kwani nimekuwa nikisaidia pia katika usafishaji wa viwanja vya mpira katika eneo hili kutokana na vijana kuomba msaada wangu, " alisema.
Hata hivyo aliiomba Serikali kuifanyia kazi kero hiyo kwani ni hatari kutokana na kuweza kusababisha madhara kwa mlipuko wa magonjwa mbalimbali.
Naye Mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho na Katibu wa Jimbo la Ukonga Bw.Juma Mwaipopo alimpongeza mlezi huyo na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano kwa kuwajibika kwa wananchi.
Alisema kuwa katika kipindi hiki si cha kupeana vitisho vya uwajibikaji bali ni ni wakati wa kuonyesha ushirikiano kwa wananchi ambao ndio walitoa dhamana kwa viongozi kuwaongoza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment