03 January 2013

Mchungaji: Umaskini unachangiwa na fikra


Na Yusuph Mussa, Lushoto

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Usharika wa Lushoto, mkoani Tanga, Daniel Shekifu, amesema umaskini wa Watazania hautokani na kukosa rasilimali bali unachangiwa na fikra zao.

Alisema Watanzania wamezungukwa na mito, maziwa, bahari, madini na misitu ambapo kama rasilimali hizo wangezitumia
vizuri, hakuna Mtanzania anayeweza kulalamikia ugumu wa
maisha bali wengi wao wameshindwa kuunganisha fikra zao
ili waondokane na umaskini kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Mchungaji Shekifu aliyasema hayo juzi katika ibada maalumu ya shukrani iliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Tanga kwa kurejea salama kutoka nchini India alipokwenda kuangalia afya yake pamoja na kumbukumbu ya
baba yake mzazi, Mzee Isaya Shekifu.

“Umaskini wetu upo vichwani wakati tuna rasilimali za kila aina ambazo kama tutazitumia vizuri ikiwemo misitu, madini na mito,
leo hii nchi ya Malawi inapambana kuhakikisha sehemu kubwa ya Ziwa Nyasa inakuwa nchini kwao kwa sababu wamebaini ndani
ya maji kuna mafuta na gesi,” alisema Mchungaji Shekifu.

Kwa upande wake, Dkt. Shekifu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo
la Lushoto, alitumia nafasi hiyo kama Mwenyekiti wa CCM mkoani humo kuwatoa wasiwasi wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

“Siwezi kukata majina yao kwa chuki bali nitatenda haki kutokana na sifa ya mgombea, uadilifu wake ndani ya chama na kuwatumikia wananchi, tukijenge chama chetu kuanzia chini.

“Kama viongozi wa chini hamtatenda haki na sisi wa juu hatuwezi lakini mimi nipo kwa ajili ya kutenda haki, umefika wakati wa wana Tanga tusahau tofauri zetu,” alisema Dkt. Shekifu.

Aliongeza kuwa, baadhi ya wana CCM walikuwa wamekata
tamaa na kuona chama hicho kimepoteza muelekeo kwa sababu
ya kutozikilizwa lakini dhamira yake ni kutaka kurudisha umoja, mshikamano na upendo.

Aliwataka Mkuu wa Wilaya hiyo, Alhaj Majid Mwanga na Mkuu
wa Wilaya ya Korogwe, Bw. Mrisho Gambo, kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kama kuna sehemu inayohitaji nguvu
ya kisiasa, wamueleze ili waweze kusaidiana.

Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na makada mbalimbali wa CCM, akiwemo Katibu wa chama hicho mkoani humo, Bw. Gustav
Muba na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani maarufu 'Majimarefu'.

Naye Bw. Ngonyani alisema hivi sasa ndani ya CCM kumejaa fitina, hivyo aliwataka wanachama waache vitendo hivyo ili chama hicho kiweze kukubalika zaidi kwa wananchi.

Bw. Muba alisema Mkoa huo upo shwari kisiasa ndio maana hata sekretarieti ya CCM imeshindwa kufika tofauti na mikoa mingine
ambayo vuguvugu la kisiasa ni kubwa.

No comments:

Post a Comment