03 January 2013

2013 uwe wa uamuzi mgumu-Lowassa


Rehema Maigala na Kassim Mahege

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Edward Lowassa, amesema mwaka 2013, kila Mtanzania anapaswa kufanya maamuzi ambayo ndio yatamwezesha kuzikabili changamoto zinazoweza kumkuta.

Bw. Lowassa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na gazeti
hili kuhusu maoni yake kwa wananchi ili waweze kuondokana na
changamoto zilizowakuta mwaka 2012.

“Kila Mtanzania anatakiwa kufanya maamuzi magumu katika mambo mbalimbali yanayoweza kujitokeza 2013 ambapo hivi sasa Watanzania wengi wanataka kupata haki zao za msingi,” alisema.

Mbunge wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro Bw. Augustino Mrema (TLP), alisema mwaka 2012 ulikuwa na changamoto nyingi ambapo Chama Kikuu cha Ushirika (KCU), kimewanyonya wakulima wa kahawa na kuhatarisha zao hilo kutoweka mkoani humo.

“Kero yangu kwa mwaka 2012, KCU imekuwa ikinunua kahawa
sh. 2,000 kwa mkopo kutoka kwa wakulima, hali hii inawafanya wawe maskini na kushindwa kupiga hatua ya maendeleo,” alisema.

Aliongeza kuwa, umefgika wakati wa Wizara husika kuona umuhimu wa kushughulikia kero hiyo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa aliwapongeza wananchi 
kwa kuanza kutambuwa haki zao za msingi.

Alisema mwaka 2012, mfumo wa vyama vingi vya siasa umewasaidia wananchi wengi kujua haki zao na kuzidai.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walilalamikia ugumu wa maisha na kuiomba Serikali ihakikishe 2013, inatekeleza wajibu wake ipasavyo na kuacha siasa katika mambo ya maendeleo
pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula.

“Bei ya vyakula inatuumiza Watanzania wa kipato cha chini, kila ukilala na kuamka, unakuta bei ya unga wa Sembe imepanda hivyo ni vigumu kuyafikia maisha bora, unga ndio chakula pekee ambacho tunakitegemea sisi walala hoi,” alisema Bi. Maimuna Musa.

No comments:

Post a Comment