29 January 2013

Maktaba sekondari ya Baobab kugharimu mil. 800



Na Rehema Maigala

SHULE ya sekondari ya Baobab iliyopo Bagamoyo Mkoani Pwani inajenga maktaba ya kisasa itakayoghalimu sh.milioni 800 ili kukidhi haja ya wanafunzi wao

Akizungumza katika mahafali ya saba ya kidato cha sita,mwishoni mwa wiki meneja wa shule hiyo Sophia Swai alisema kuwa,wameamua kujenga maktaba hiyo ili kukidhi haja ya wanafunzi na vilevile kuongeza idadi kubwa ya ufulu kwa wanafunzi.

Alisema kuwa shule yao ni ya wasichana hivyo wanahaja kubwa ya kufaulisha watoto wa kike kwa kuwa ukimwelimisha mtoto wa kike umeimalisha jamii nzima

"Tunajenga maktaba hii na tunatarajia kuongeza vitabu 2000 kila mwanzo wa mwaka kufuatana na mahitaji na ongezeko la wanafunzi "alisema Swai.

Aliongeza kuwa tayari shule hiyo imepata mkopo wa sh.milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo na kwa gharama iliyobaki wanatafuta msaada au mikopo nafuu kutoka kwenye mabenki na taasisi mbalimbali.

Alisema kuwa kwa sasa hivi shule ina maktaba yenye vitabu 11400 vya kiada na ziada ambavyo kwa wanafunzi tulionao vinatosheleza.

Vilevile alisema kuwa shule ina maabara nne ya fizikia, kemia, baolojia na maabara zote vina vifaa vya kutosha kuwawesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo ili kuongeza ufahamu wao katika masomo ya sayansi.

Naye,MKurugenzi wa shule hiyo Alphan Swai alisema kuwa,sera ya shule yake ni ni kumuelimisha mtoto wa kike ambaye atajitegemea katika maisha yake kifikra,kiuchumi na kijamii katika hali ya sasa ilivyo.

Alisema kuwa shule yake inasajili wanafunzi wenye alama za kuanzia asilimia 30 katika somo la hisabati na 50 katika masomo ya lugha na maarifa.

Aliongeza kuwa jumla ya wanafunzi 140 wa kidato cha sita wanatarajiwa kufanya mitihani ya kumaliza kidato cha sita Februali mwaka huu.

No comments:

Post a Comment