14 January 2013

Makalla amwaga misaada mvomero


Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamepatiwa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 2.5.

Msaada huo umetolewa jana na Mbunge wa Mvomero ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Amos Makalla wakati wa ziara yake ya siku tatu ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo katika jimbo hilo.

Msaada alioutoa ni pamoja na vitanda, magodoro, shuka za wagonjwa kwa zahanati ya kijiji cha Matale pamoja na madawati 25 kwa shule ya msingi Kinda wilayani Mvomero.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Bw. Makalla alisema kuwa madawati hayo yenye thamani ya sh. milioni ameyatoa baada ya kuona mazingira ya shule hiyo ya Kinda wanafunzi kukaa chini wakati alipokuwa katika kampeni za uchaguzi mwaka juzi.

Bw. Makalla alisema alifanya mkutano hapo shuleni wakati wa uchaguzi wa ubunge wa ndani ya CCM, hali ya shule ilimsikitisha ikiwa ni pamoja na watoto kuwaona wakisoma huku wakiwa wamekaa chini.

"Nilisikitika sana moyoni nikasema  nikipata ubunge lazima nisaidie hii shule, hivyo nimeanza na madawati na vingine vitafuata,"alisema.

Bw. Makalla pia alikabidhi msaada wa vitanda, magodoro na mashuka yenye thamani ya sh.milioni moja katika kijiji cha Matale Kata ya Mvomero.

Mbunge huyo alisema kuwa aliamua kutoa msaada huo baada ya kuombwa na wananchi wa kijiji hicho mwezi mmoja uliopita wakati wakati alipokuwa katika ziara jimboni humo.

No comments:

Post a Comment