31 January 2013

KESI YA PONDA KUENDELEA LEO

Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo inatarajiwa kuendelea na kesi ya wizi na uchochezi inayomkabili Katibu  wa Jumuiya na Taasisi za  Kiislam  Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake kutokana na upande wa mashtaka kukosa mashahidi.


Kesi hiyo inayosikilizwa mbele ya Hakimu Victoria Nongwa leo upande wa serikali unaowakilishwa na wakili Tumaini Kweka unatarajiwa kuleta shahidi wake wa saba.

Mashahidi ambao tayari walishatoa ushahidi wao katika kesi hiyo ni pamoja na  Katibu Mkuu wa Bakwata Sheikh Said Golila,Sheikh Ismail Habibu ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mkurugenzi wa Kampuni ya Agritanza Bw.Suleiman Mohamed.

Wengine ni Bw.Masoud Ikome ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhmanini Bakwata ,Bw.Hafidhi Othuman Meneja Uujenzi wa Kampuni ya Agritanza.

Katika kesi hiyo,Oktoba 18 mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka manne isipokuwa Sheikh Ponda .

Wakili Mwandamizi wa Serikali Kweka alidai washitakiwa 49 wanakabiliwa na makosa manne na Ponda ana kabiliwa na makosa matano.

Makosa hayo ni kula njama kutenda kosa ,kuingia kwa nguvu kwa nia ya kutenda kosa ambapo ilidaiwa kuwa Oktoba 12 mwaka huu huko Chang’ombe Markasi, pasipokuwa na sababu za msingi washtakiwa hao waliingia kwa jinai kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya  Agritanza.

Kosa lingine ni kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya  Agritanza.

Lingine ni la  uchochezi ambalo linamkabili Sheikh Ponda na Sheikh Mkadam ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 12 mwaka huu,katika eneo la Chang'ombe Markaz  waliwashawishi washitakiwa hao watende kosa hayo.

No comments:

Post a Comment