28 January 2013

Kalonga waikataa taarifa ya tume


Na Suleiman Abeid,
Shinyanga

WAKAZI wa mtaa wa Kalonga manispaa ya Shinyanga wameikataa taarifa ya Tume ya uchunguzi iliyokuwa imeundwa kuchunguza ubadhirifu wa shilingi milioni 26.2 zilizokuwa zimetolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa barabara katika mtaa huo,ambapo pia mradi ulilenga kuwasaidia wakazi wa mtaa huo kujipatia kipato waliokuwa wakikabiliwa na uhaba wa chakula kitakachowawezesha kujinunulia chakula.

Hata hivyo wakati mradi huo ukitekelezwa ilibainika kuwa baadhi ya watu walioteuliwa kuusimamia walituhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha hizo hali iliyosababisha iundwe Tume ya uchunguzi ili kubaini kama kweli palikuwepo na ubadhirifu uliotajwa.

Kutokana na hali hiyo wakazi hao waliunda tume ya watu sita ambapo uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga uliwaongezea wataalamu wawili akiwemo mkaguzi wa ndani Mussa Singu na mwenzake aliyetajwa kwa jina la Msafiri na kuwa timu ya watu
wanane.

Baada ya tume kukamilisha uchunguzi wake ulifanyika mkutano wa hadhara uliowajumuisha wakazi wote wa mtaa huo kwa lengo la kupokea taarifa ya tume hiyo,
ambapo ilielezwa kuwa katika uchunguzi huo ilibainika kiasi cha fedha kilichofujwa
kilikuwa ni shilingi milioni 5.8 na siyo milioni 26.2 kama ilivyodaiwa hapo awali.

Akisoma taarifa hiyo mkaguzi wa ndani, Singu aliwaeleza wakazi hao kwamba tume ilibaini chanzo cha ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha kilisababishwa na uzembe wa Kamati ya usimamizi wa mradi na kwamba tume kwa upande wake ilipendekeza kurudiwa upya kwa kazi ya ukarabati wa barabara hiyo.

Hata hivyo aliyekuwa katibu wa tume, Mohamed Bulemo alisimama na kupinga vikali kwamba taarifa iliyosomwa kwa wananchi na mkazi huyo haikuwa sahihi baada ya kuficha baadhi ya mambo na kwamba yeye anachofahamu ubadhirifu uliobainika katika uchunguzi wao ulikuwa ni kiasi cha shilingi 26,218,750.

Hali hiyo ilisababisha wananchi kuchachamaa na kuikataa taarifa iliyosomwa na mkaguzi huyo baada ya kuelezwa kuwa wakati uchunguzi ukiendelea tume iligawanyika katika makundi mawili ambapo wataalamu kutoka Manispaa waliwabagua wajumbe wengine
kwa madai ya kwamba hawakusoma na hawajui kitu.

Mmoja wa wakazi wa mtaa huo Boniphace Shola alielezea kushangazwa kwake na jinsi wataalamu waliokuwa wakitegemewa kufichua ukweli kuchangia kuficha madhambi yaliyojitokeza na kwamba kitendo walichokifanya kilikuwa ni kinyume na maadili ya
kazi yao.

“Hawa wasomi ndiyo wametuletea shida hapa, hatuwahitaji tena kwa sababu hakuna
walichokifanya hata kimoja, tulitegemea watatuletea majibu mazuri kumbe na wao hakuna kitu, hii taarifa hatuitaki na badala yake tutafanyia kazi taarifa iliyosomwa na katibu wa tume na kisha tupate mkaguzi wa nje achunguze zaidi,” alisema

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo, Sebastian Peter “Obama” aliwaomba wakazi hao kufanya subira bila na wasichukue maamuzi yoyote yenye jazba na kwamba yeye binafsi atahakikisha anafuatilia kwa undani suala hilo na atatafuta mkaguzi kutoka nje ili apitie hesabu zote na ukweli uweze kufahamika.


No comments:

Post a Comment