21 January 2013

Jiji kuandaa ramani,ujenzi wa kituo cha mabasi Mbezi



Na Heri Shaaban

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam inaandaa mchoro wa ramani kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo Mikoani na Nchi Jirani eneo la Mbezi kwa Ruis.


Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana, na  Mkurungenzi wa Jiji hilo Mussa Zungiza  wakati wa kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea mikakati ya jiji baada kumaliza zoezi la kuwaondoa wafanyabishara ndani ya kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo.

Zungiza alisema kuwa kwa sasa timu yake ya jiji hipo na Washauri Wataalam kwa ajili ya kuweka michoro ya ramani ya ujenzi wa kituo cha kisasa kitakacho chukua magari mengi.

"Kituo hichi kipya cha mabasi ya mikoani na nchi jirani kitakuwa cha kisasa na kitakuwa na uwezo wa kuchukua magari zaidi ya 600"alisema Zungiza.

Alisema kuwa mara baada kumaliza kuweka michoro ya ramani hatua itakayofuata ni ujenzi wa awali kwa ajili ya kuboresha miundombinu,vyoo, sehemu ya kupaki magari na ya hoteli kwa ajili ya wasafiri.


Aidha Zungiza alisema kuwa mradi huo wa kituo cha mabasi unatarajia kukamilika mapema ambapo kwa sasa halmashauri hiyo na wataalam wapo katika vikao vya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi ili malengo yaliokusudiwa yafanikiwe na usikwamishe shughuli za kijamii.

Alisema kuwa mara baada hatua za kuboresha miundombinu ya kituo hicho kukamilika Mbezi kwa Ruis, hatua itakayofuata ni kuonana na Wamiliki wa mabasi ili waweze  kuondoa mabasi yao eneo la Ubungo.

Eneo la kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo awali ilikuwa eneo la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA)kabla Serikali kubadilisha matumizi yake na kuwa kituo cha mabasi ya kwenda mikoani na nchi jirani.

Hata hivyo  serikali hiyo hiyo imebadilisha  matumizi ya kituo cha mabasi ya mikoani na kuwa kituo cha magari ya mwendo kasi DART mradi unaotarajia kukamilika mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment