07 January 2013

'Hakuna sayari tishio kwa dunia'


Na Danny Matiko

WATAALAMU wa masuala ya anga za juu na pia wale wa Shirika la Safari za Anga za Juu la Marekani (NASA) wamekanusha uvumi ambao unaenezwa na baadhi ya watu kwamba kuna sayari imepoteza mwelekeo wake, na kwamba ipo njiani kuja kuigonga dunia na kuangamiza viumbe wake, tukiwemo wanadamu.


Kadhalika, kama kwamba hiyo haitoshi, dawati la makala haya limekuwa likipokea ujumbe kutoka kwa baadhi ya wasomaji wetu wakiulizia kama kuna ukweli kuhusu madai kwamba mawimbi hatari ya miale ya sumu kutoka sayari nyekundu ya Mars yanakuja duniani, na kwamba mawimbi hayo yana uwezo wa kusababisha maradhi ya kansa ya ngozi.

Pia, hivi karibuni mwandishi huyu alipokea ujumbe mfupi wa simu (sms) ya kiganjani kutoka kwa ndugu, ukimshauri kuweka mbali simu usiku ili kuepuka kudhuriwa na mawimbi hayo ya sumu kutoka Mars.

Ujumbe huo ambao ulioonesha kuwa ni nukuu ya tahadhari kutoka NASA na BBC, ulimaanisha kuwa mawimbi hayo ya sumu kutoka Mars yalikuwa yakisafiri kwa kupitia masafa ya simu, na hivyo kwa kupitia kwenye simu yangebadilika na kuwa mionzi hatari kwa mtumiaji wa simu.

Hakika kwa kadiri tunavyofahamu sayansi ya anga pamoja na jinsi mawimbi ya nguvu za asili yanavyosafiri, uvumi huo haukuwa na ukweli wowote, kwani dunia imekingwa na utando wa anga unaozuia vitu vyepesi, kama mawimbi ya mionzi hatari kutoka anga za juu kuweza kupenya na kutua duniani.

Utando huo ambao ni uwanda mpana wa anga, huweza kusambaratisha vitu vinavyotaka kuingia kinyemela duniani kutoka angani.

Uwanda huo mnene umetanda pande zote za duara ya dunia kuanzia umbali kilometa 15 hivi kutoka ardhini kwenda juu na kuendelea mpaka umbali wa kilometa 40 hivi angani, ambako pia uwanda huo nao umekingwa na hali ya hewa yenye joto kali la kuweza kuyeyusha chuma au jiwe linaloanguka kutoka anga za juu.

Msomaji, kukumbuka kuwa wastani wa umbali kutoka kwenye jua mpaka duniani ni kilometa milioni 150, na kwamba jua hutema kuja duniani asilimia 100 ya miale yake yenye mionzi hatari ya sumu.

Mionzi hiyo husafiri pamoja na mwanga mkali kuja duniani na kuwasili ndani ya dakika 8 na sekunde 19, lakini kabla ya kutua duniani asilimia 98 ya mionzi hiyo huchujwa na kusambaratishwa angani na kushindwa kupenya uwanda huo unaoikinga dunia.

Hii ikiwa na maana kwamba ni asilimia 2 ya hiyo mionzi hatari ya jua ndio hupenya na kutua duniani.

Tunaona kwamba katika hali ya kawaida ingetarajiwa kuwa kasi hiyo kubwa ya miale ya jua,ingetosha kupenya kwa urahisi uwanda wa utando unaoikinga dunia na kutua moja kwa moja duniani.

Hivyo basi, hili joto la jua na mwanga wake vinavyotua duniani, huwa tayari vimechujwa kwa kiwango cha juu na kuondolewa sumu hatari kwa ngozi ya binadamu.

Sasa kama ukali wote huo wa miale na mwanga wa jua pamoja na mawimbi yanayovisafirisha huzuiwa na "kinga" hiyo imara ya dunia, je, ingewezekana vipi miale dhaifu yenye mionzi ya sumu kutoka sayari ya Mars kuweza kupenya kinga hiyo na kuingia duniani na kuleta madhara?

Ni kwamba hali hiyo haiwezekani kutokea kwa sasa, labda pale ambapo shughuli za kibinadamu, kama vile uchafuzi wa mazingira ya anga, zitakopokuwa zimeathiri kwa kiasi kikubwa mno uimara wa utando huo wa anga, ambao unafahamika kisayansi kama "Ozone Layer."

Hivyo basi, uvumi unaoenezwa kuwa kuna mawimbi ya mionzi ya sumu kutoka sayari ya Mars kuja duniani ni uongo na udanganyifu mtupu.

Pengine tusema tu kwamba dunia, tofauti na sayari zingine 8 ambazo hujiendesha kwa kutumia nguvu asili ya uvutano, imepewa upendeleo wa kiasili ambao pia ni ulinzi kwa viumbe wake wote.

Kwa upande wa kuwepo mwisho wa dunia kutokana na dunia kugongwa na sayari nyingine, madai hayo nayo si sahihi, kwani hakuna sayari inayoweza kukurupuka au kupoteza mwelekeo wake na kuja kuigonga dunia bila kuonekana miaka kadhaa mapema.

Hebu ngoja tuangalie ukweli huo kwa viegezo kadhaa ambavyo vinatupatia nguvu na sababu za kutoamini kuwepo kwa mwisho wa dunia kwa kugongwa na sayari nyingine.

Ni kwamba kama kweli ungekuwepo ujio wa sayari nyingine kwenye anga ya dunia, na pia hata kama mashirika yanayochunguza anga za juu yangeamua kula njama na kuficha ukweli wa ujio huo, ni dhahiri kuwa kwa sasa sayari hiyo ingekuwa inaonekana kwa macho iking'aa sana angani, hususan nyakati za usiku.

Kadhalika, jambo ambalo haliwezekani kutokea ni kwamba sayari haiwezi kupotoka kutoka katika muhimili wake na kusafiri haraka kuja kuigonga dunia bila kuonekana takribani miaka 10 kabla ya kufika duniani.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba kanuni ya hesabu za umbali mkubwa unaozitenganisa sayari hairuhusu hali hiyo kuweza kutokea.

Kutokana na mazingira hayo ya anga kuwa na upana usio na mwisho, haiwezekani kabisa tukaingia kulala bila kuwepo dalili yoyote ya kutisha angani na ghafla tu asubuhi yake tukaona sayari nyingine ikija kuigonga dunia.

Hiyo pia ni kwa kuwa hakuna sayari yenye kasi ya namna hiyo, kwani hata chombo cha Apollo kilicho kwenda kutua mwezini mwaka 1969, licha ya kuwa na mwendo-kasi kilometa 40,000 kwa saa, bado kilisafiri kwenda huko kwa siku 4.

Pia umbali kutoka duniani kwenda sayari ya Mars ni kilometa milioni 225, ambapo chombo cha "Curiosity" kutoka duniani kiliweza kuchana anga hiyo kwa miezi takribani 8 kuweza kufika huko.

Ni vyema tuwaulize wadanganyifu hao watuambie hiyo sayari inayokuja kuigonga dunia ilionekana lini, kwani viona mbali vya kimataifa vinachunga anga muda wote wa 24, na isitoshe, viona mbali hivyo vinapenya mpaka kuona kingo za inapoishia anga ya jua na inapoanzia anga ya mbali (deep space) na kuendelea.

Kwa upande wa sayari "X" inayotajwa kwamba ndo inakuja kuigonga dunia, licha ya Mataifa Makubwa kukanusha uwepo wa sayari hiyo, inadaiwa na wachunguzi binafsi wa anga kuwa kwa sasa ipo nyuma ya jua na hivyo kutoonekana kwa rahis.

Inadaiwa kuwa sayari hiyo ipo umbali wa kilometa bilioni 81 kutoka duniani, ambapo umbali huo mkubwa ni tosha kuwa ushahidi kwamba hata katika kipindi cha miaka 10 ijayo  sayari hiyo itakuwa bado ipo mbali na hivyo kutokuwa tishio kwa dunia.

Shirika la Safari za Anga za Juu la Marekani (NASA) ambalo ni chombo cha serikali ya Marekani kinachoratibu safari za uchunguzi wa anga, mara kadhaa limekuwa likikanusha uvumi wa kuwepo sayari hiyo ambayo ukubwa wake inadaiwa kuwa ni mara 5 zaidi ya ukubwa wa dunia.

NASA imekuwa ikikanusha madai ya kuwepo sayari ya aina hiyo, ambapo baadhi ya raia wa nchi hiyo wanaituhumu serikali yao kwamba inaficha ukweli kuhusu uwepo wa sayari hiyo inayojulikana kwa jina la Nibiru.

Shirika hilo lilisema katika taarifa rasmi siku chache kabla ya Desemba 21, mwaka jana, kwamba wanaoeneza habari hizo za sayari ya "X" ni waongo, ambao wana lengo la kuwatisha walimwengu bila sababu yaoyote.

  Tahadhari hiyo inafuatia habari ambazo zimekuwa zikienezwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo kwa kupitia mitandao ya kompyuta na pia baadhi ya watu wenye 'nafasi' za kuweza kusikilizwa na jamii, ikidaiwa kwamba dunia ingepatwa na janga kubwa kutoka angani siku ya Desemba 21, 2012, jambo ambalo limethibitika kuwa udanganyifu mtupu.

  Kutokana na kuenea kwa udanganyifu wa aina hiyo, ni vyema jamii kujiamini na kutokuwa na hofu wala woga, kwani wanaoeneza uvumi huo wanakuwa na ajenda zao za kibinafsi.

No comments:

Post a Comment