07 January 2013

China itaongoza uchumi wa dunia?


Na Danny Matiko

JUMAPILI iliyopita tuliangalia jinsi taifa la China lilivyokumbwa na migogoro ya kijeshi na kisiasa kwa miaka mingi, na kusababisha kusambaratika kwa maendeleo yake yote ya kale.


Kutokana na mifarakano hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, waliibuka wababe wa kivita kama ilivyo Somalia, Barani Afrika, ambapo serikali ya nchi hiyo wakati huo ikijulikana kama Jamhuri ya China, ilishindwa kupata suluhu ya mgogoro huo.

Tuliishia kuona Bw. Mao Zedong akiwa ameibuka kutoka miongoni mwa vijana wafuasi wa "Chama cha Kikomunisti" ambacho kilikuwa dhaifu, ikilinganishwa na chama tawala cha "Nationalist".

Mao na wanamgambo wenzake wa Kikomunist wakiwa "wamepigwa msasa" wa kisiasa na makamanda wa Kirusi na kukubali kuuunganishwa na wanamgambo wa "Nationalist" na kuunda jeshi la pamoja la kitaifa la serikali, walikwenda Kaskazini mwa nchi hiyo kupambana na waasi.

Lakini,wakiwa huko mstari wa mbele dhidi ya waasi hao,maarufu kama wababe wa kivita, ghafla waligeukwa na "Nationalist" na kushambuliwa huko kwenye uwanja wa mapambano.

Historia inaonesha kuwa serikali ya chama tawala cha "Nationalist" iliamua kukomesha siasa za Kikomunist, ambapo ilianzishwa kampeni ya kuwaondoa kutoka jeshini wafuasi wote na wanachama wa Chama cha Kikomunisti ambacho kilikuwa na urafiki na Urusi.

Kampeni hiyo ya ghafla pia ilivunja ushirikiano kati ya serikali hiyo ya Jamhuri ya China na Urusi kutokana na kuvurugika kwa hali ya mambo kati ya vyama hivyo viwili.

Ilipotimu Aprili 12,1927 msako dhidi ya Wakomunisti uliendeshwa makambini ambapo jumla yao 1,000 walikamatwa,300 walinyongwa na 5,000 kudaiwa kupotea.

Kutokana na tukio hilo, na mengineyo mengi ya aina hiyo, akina Mao waliamua kujiondoa kwenye umoja huo wa kitaifa na kukimbilia mpakani mwa Urusi ambako walipata msaada ambao hatimaye uliiangusha serikali ya "Nationalist."

Kuna matukio mengi hapo katikati ambayo yalijiri mpaka akina Mao kushinda vita hiyo ya miaka zaidi ya 20 kati ya wenyewe kwa wenyewe, kuanzia mwaka huo wa 1927 mpaka 1949.

Kufuatia kutimuliwa kutoka madarakani serikali ya Jamhuri ya China iliyoongozwa na chama cha "Nationalist," na kuamua kukimbilia kisiwani Taiwan, ukombozi huo mpya ndio uliunda "Jamhuri ya Watu wa China", ambapo Mao Zedong aliteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Jamhuri hiyo mpya.

Mataifa ya Magharibi kama kawaida yakiongozwa na Marekani, yalilaani mno kuenguliwa kwa serikali ya chama tawala cha "Nationalist," ambacho siasa zake zilikuwa za mrengo wa Kimagharibi.

Kwa kuwa serikali iliyoondolewa na akina Mao ilikuwa tayari ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UNO), umoja huo uligoma kuitambua Jamhuri mpya ya watu wa China chini ya mwenyekiti wake, Mao.

Nchi karibu zote za dunia,isipokuwa Urusi na nchi chache,ndizo ziliitambua Jamhuri hiyo mpya ya Watu wa China, ambapo sehemu kubwa ya mataifa yalidai kurejeshwa kwa "Wanationalists."

Hivyo basi, China "mpya" kama ilivyokuwa ikifahamika kisiasa ilianza kujijenga chini ya Chama cha Kikomunisti cha China, huku Mao akiwa mwenyekiti wake.

Hakika, Mao na Wakomunisti wenzake walishika hatamu ya mambo yote kuanzia madogo mpaka makubwa, ambapo kila mwananchi alitakiwa kufanyakazi kwa bidii ili kuikwamua kiuchumi nchi "mpya."

Kazi za kilimo na uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo ili kukidhi mahitaji muhimu kwa umma, ni baadhi ya vitu vilivyopewa kipaumbele, lakini pia bila kusahau sekta kama za afya na elimu kwa wananchi wote.

Mojawapo ya nyenzo alizozitumia Mao katika ujenzi wa nchi mpya ni pamoja na Jeshi Jekundu la nchi hiyo, ambalo lilisimamia nguvukazi kutoka upande wa wananchi.

Katika hali ya namna hiyo ambapo taifa liliamua kusonga mbele kwa kauli moja, vitendo vya kihalifu, kama ufisadi, rushwa, na kutokuwajibika vilipungua na kutoweka kwa kiwango chake, kwani adhabu zilikuwa ni kali.

Mataifa ya Magharibi, kama ilivyo ada, pamoja na jumuiya zake yalilaani serikali ya China kwa kukiuka haki za binadamu, ambapo ilionekana kama serikali ya Kikomunisti ya nchi hiyo iziba masikio na kukaza buti dhidi ya uhalifu.

Hivyo, tunapoiona China ikiwa mbioni kutaka kukamata uchumi wa dunia, si suala la kubahatisha, bali ni kutokana na juhudi za serikali, hususan viongozi katika ngazi zote.

Hebu ngoja tuangalie vionjo vya baadhi ya mamia ya semi za Mao ambazo alitumia katika kuhamasisha wananchi wake katiaka ujenzi wa taifa hilo:-

"Misuguano ya kisiasa kati ya pande mbili zinazopingana katika jamii husaidia kusukuma mbele maendeleo katika jamii husika; misuguano hiyo ndiyo huondoa mfumo wa kizamani usio wa kimaendeleo, na kuleta mfumo mpya wa maendeleo na hivyo kuwezesha jamii kusonga mbele."

"Sisi ni wapenda amani, lakini, hata hivyo, kama Mataifa ya Magharibi na marafiki zao wanataka kuanzisha vita tutakuwa hatuna njia ya kukwepa isipokuwa ni kupambana nao katika vita kamili mpaka mwisho; halafu tutarejea kuendelea na ujenzi wa taifa letu."

Kadhalika, katika kuelekea kwenye maendeleo, tangu mwanzo katika uongozi wa kiongozi huyo mahiri, msisitizo wa serikali yake uliwekwa katika kuhakikisha kuwepo chakula cha kutosha kwa raia wote wa nchi hiyo, afya kwa umma, na elimu kwa wananchi wote.

Hiyo ilitokana na serikali ya nchi hiyo kudai kuwa bila shibe ya kutosha wananchi watashindwa kufanyakazi za maendeleo, na kadhalika bila kuwepo afya bora nchi hiyo itakuwa kama taifa la watu wagonjwa wasioweza kufanyakazi za maendeleo, na pia bila elimu nchi itakuwa ya watu wajinga ambao itakuwa vigumu kwao kujitambua na hivyo kutokuwa wazalendo.

Sekta hizo za kilimo, afya, na elimu zilipewa umuhimu wa kwanza katika taifa hilo, ambapo pia kila familia ilitakiwa kufuata mpango wa uzazi ili kudhibiti mfumuko wa kuzaliana ovyo.

Hata hivyo, ingawa nchi hiyo inakazania kutaka kuipiku Marekani kiuchumi kuna shaka kwamba Mataifa ya Magharibi hayatakubali hilo litokee.

Ingawa mataifa hayo kwa sasa yanaendelea kuhamisha mitaji yao mingi ya kibiashara kwenda nchini humo, miaka michache ijayo yatagundua kuwa yamefanya makosa, kwani mitaji hiyo ndiyo imekuza kwa kiwango cha juu uchumi wa China.

Kuna uwezekano mataifa hayo yakaondoa mitaji hiyo taratibu na kuirejesha Ulaya, ingawa kwa kufanya hivyo si suluhisho kwani bado teknolojia itasalia nchini humo na hivyo kuendelezwa na raia wazawa wa China.

Mpaka hapa, ni suala la kusubiri kuona kitakachotokea, na hasa ikizingatiwa kuwa hata kama bidhaa za nchi hiyo zitapigwa maruku kuingia Ulaya na Marekani, Wachina wamekamata soka la Afrika, Latini Amerika na Asia.

Isitoshe, eneo ambalo China ipo, ndilo kitovu cha amani ya dunia, tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa ni Mashariki ya Kati.

Katika eneo hilo mataifa yote yanatazamana kwa shaka, kwani kila taifa lina kumbukumbu mbaya ya kihistora dhidhi ya mwenzake kufuatia matukio ya historia ya nyuma ambayo ndiyo yaliidhoofisha nchi hiyo kiuchumi, kisiasa, na kijeshi, ambapo pia imetumia takribani miaka 60 kurejea tena upya katika ulingo wa kimataifa.

Mataifa hayo ambayo yanapakana kwa kutenganishwa na bahari katika eneo hilo nyeti ni China yenyewe, Japani, Korea zote mbili (Kaskazini na Kusini), Urusi, Vietnam, na Marekani ambayo pia inaungwa mkono na nchi washirika wake wa Ulaya katika Umoja wao wa Kujihami (NATO).

No comments:

Post a Comment