21 January 2013

Fenella ataka vijana wapige vita dawa za kulevya


Na Amina Athumani

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mkangara amewataka wachezaji wanaocheza wa Kombe la Meya kuwa mabalozi wazuri katika kupiga vita utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, wakati wa uzinduzi wa kombe hilo lililoandaliwa na kudhaminiwa na Benki ya NMB, Waziri Fenella alisema vijana ni nguvu kazi ya taifa hivyo wasingependa kuona wanateketea kwa dawa za kulevya na kufanya vitendo vya kihalifu.

Alisema Wizara yake ambayo ina jukumu la kusimamia michezo pamoja na vijana itahakikisha kampeni ya mashindano hayo ya kuhamasisha usafi na ulinzi shirikishi inafanikiwa na ujumbe huo kuwafikia vijana wengi kupitia michezo.

Waziri Fenella ameipongeza benki ya NMB kwa kuweza kuandaa na kudhamini mashindano hayo ambayo yamekusanya vijana kutoka kata 34 za Halmashauri ya Kinondoni.

Waziri huyo pia amewapa changamoto waandaaji wa kombe hilo kuhakikisha wanaandaa Ligi ya wanawake kwa kuwa soka la wanawake nalo linakuja kwa kasi.

"Safari ijayo nataka munialike kuja kuzindua kombe la mpira wa miguu kwa wanawake naamini hilo litawezekana na tutaweza kuibua vipaji bora kupitia michuano hiyo,"alisema Waziri Fenella.

Michuano hiyo ilianza ngazi ya Diwani Cup ambapo kwa sasa imeingia hatua ya Meya Cup ambapo mshindi atapata zawadi mbalimbali ikiwemo pikipiki aina ya TVS King yenye thamani ya sh. milioni 6 itakayotolewa kwa mshindi wa kwanza.

No comments:

Post a Comment