03 January 2013

Dkt. Shein: Amani ndio msingi wa neema


Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.
Ali Mohamed Shein, amewahakikishia wananchi kuwa neema, baraka na mafanikio zaidi, yatapatikana nchini kama wananchi wataona umuhimu wa kushikamana, kusimamia amani, utulivu pamoja na kufanya shughuli halali za kujipatia kipato.

Taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema Dkt. Shein aliyasema hayo Ikulu, mjini Zanzibar jana wakati akitoa salamu za kuukaribisha mwaka 2013 kwa wananchi.

Dkt. Shein alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo kiuchumi, kijamii, miundombinu na huduma za jamii kama afya, elimu, upatikanaji maji safi na salama, pamoja na chakula cha kutosha kutokana na juhudi za wakuliwa na wafanyabiashara.

Alisema ukuaji wa maendeleo katika nchi yoyote duniani hutegemea hali ya amani na utulivu ambapo vyombo vya ulinzi na usalama, vimeweza kuidhibiti hali hiyo.

“Natoa pole kwa Wazanzibari wote walioathirika kutokana na vitendo vya ghasia na uvunjaji wa amani vilivyosababisha hasara kubwa na usumbufu kwa wananchi.

“Navipongeza vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuimarisha hali ya amani na utulivu nchini, nawaomba wananchi muendelee kushirikiana na Serikali kuzuia vitendo vyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani,” alisema.

Dkt. Shein alisema Zanzibar imeendelea kujijengea taswira njema kwa marafiki na taasisi mbalimbali za kimataifa kutokana na mafanikio yaliopatikana baada ya kuanzishwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.

Alisema kutokana na hali hiyo ni vyema mafanikio hayo yakazidi kuendelezwa kwa faida ya kila mmoja, kuzidi kuaminiana pamoja
na kuongeza ushirikiano.

Katika salamu hizo, Dkt. Shein aliwakumbusha wananchi wajibu wao wa kulinda miundombinu iliyojengwa kwa gharama kubwa zikiwemo barabara, nguzo za umeme pamoja na waya.

Aliwataka wananchi wote kuwa walinzi wa rasilimali ziliopo na kuzingatia sheria katika matumizi bora ya rasilimali hizo kwa
faida yao na vizazi vijavyo.

No comments:

Post a Comment