03 January 2013

Diwani CCM Mara ahamia CHADEMA



Na Timothy Itembe, Rorya

DIWANI mstaafu wa Kata ya Rorya-Tarime, mkoani Mara,
Bw. Osolo Silasi, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na wenzake wawili, juzi walitangaza kukihama chama hicho na
kuhamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Bw. Silasi na wenzake walitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Nyambogo wakati Diwani wa Kata ya Kitembe, Bw. Thomasi Patrick (CHADEMA), akisoma taarifa ya miradi ya wananchi aliyoitekeleza baada ya kushika nafasi hiyo.

Alisema baada ya wananchi kumpa dhamana ya kuwa diwani wao, amefanikiwa kutekeleza ahadi zake ambazo ni pamoja kuisafisha
Barabara ya Raranya, Nyambogo hadi Obwere.

“Nimefanikiwa kutekelezaha ahadi hii kwa ushirikiano wa wananchi pamoja na Mbunge wa Rorya, Bw. Lameck Airo aliyetoa katapila la ambalo limetumika kuzibua barabara hizi ambazo zinapitika kirahisi hivyo wananchi wameweza kunufaika kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake, Bw. Silasi alisema amelazimika kuhamia CHADEMA kwa madai kuwa, viongozi wengi CCM wameingia madarakani kwa rushwa hivyo wananchi kukosa haki ya msingi.

“Tangu uhuru wakati kata hii ikiongozwa na CCM, hakukuwa na barabara kutoka Nyambogo Raranya hadi Obwere na kusababisha wagonjwa wengi kupoteza maisha njiani wakiwa wanapelekwa Hospitali ya Obwere (Shirati), kwa matibabu hasa wanawake waliokuwa wakienda kujifungua,” alisema.

Aliongeza kuwa, tangu Bw. Patrick achaguliwe kuwa diwani wa kata hiyo, amefanya mambo mengi ya mendeleo na kukomesha wizi mkubwa wa mifugo ya wananchi.

Wanachama wengine wa CCM waliohamia CHADEMA ni pamoja na Bw. Mikoro Yoko ambaye amekitumikia chama tawala miaka 15 kama Balozi wa Kitongoji.

Mwingine ni Bw. Chiro Ndege ambaye alisema CCM haina sera
kwani kila kukicha bei ya bidhaa mbalimbali zinapanda hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CHADEMA, wilayani Tarime, Lukasi Ngoto, alisema kazi inayofanywa na chama chake ni kutoa elimu kwa wananchi ili wafanye uamuzi wenyewe.

No comments:

Post a Comment