04 January 2013
Diwani CCM Kortini kwa kujipatia mil. 31/-
Na Rehema Mohamed
ALIYEKUWA Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata
ya Makumbusho, Dar es Salaam, Bw. Christopher Mutayoba, jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kujipatia sh. milioni 31 kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali Lucy Diganyeki, mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Wakili Diganyeki alidai mahakamani hapo kuwa, katika shtaka
la kwanza, kati ya Agosti 22 na Oktoba 25,2011, sehemu isiyofahamika jijini Dar es Salaam, alighushi hati ya makazi
kuonesha Bw. Samson Laizer na Bi. Suzy Laizer, wana haki ya kumiliki kiwanja namba 253 kilichopo Bahari Beach, eneo la Manispaa ya Kinondoni.
Shtaka la pili, ilidaiwa kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa huyo alighushi ramani kuonesha Manispaa ya Kinondoni, imeitoa kiwanja hicho kwa Bw. Samson na Bi. Laizer, huku akijua si kweli.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kuwasilisha hati ya kughushi kosa analodaiwa kulitenda Septemba 7,2011, Ofisi za Ardhi kuonesha kwamba ni nyaraka halali na imeandaliwa na Manispaa ya Kinondoni.
Shtaka la nne ilidaiwa Desemba 30, 2011, sehemu tofauti jijini Dar es Salaam, alijipatia sh. milioni 31, kutoka kwa Bw. Samson na Bi. Laizer kwa ajili ya kuwawezesha kupata eneo hilo.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo ambapo Hakimu Riwa alisema dhamana yake ipo wazi ambapo kesi hiyo itatajwa Januari 17, mwaka huu. Mshtakiwa amerudishwa rumande.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment