07 January 2013

Chawapimbi chatakiwa kujikita kwenye miradi


Na Kassian Nyandindi,Mbinga.

CHAMA cha Waendesha Pikipiki wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma(CHAWAPIMBI) kimetakiwa kujikita katika uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili wanachama wake wajikwamue kiuchumi.


Rai hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Mkoa huo Oddo Mwisho alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho katika ukumbi wa Tulivu uliopo mjini hapa jana.

Mwisho alisema kitendo cha waendesha pikipiki hao kuanzisha umoja huo ni suala la kuigwa na la mfano kutokana na hivi sasa vijana hao wanaouwezo wa kukopesheka hata na vyombo vya kifedha ikiwemo benki hasa kama watajikita katika uanzishaji wa miradi.

Alisema pikipiki zimekuwa zikiajiri vijana wengi ambao awali walikuwa hawana kazi hivyo ni jambo la msingi ni kwa kila mwendesha pikipiki kuhakikisha anafanya kazi yake ya kila siku kwa umakini, ikiwemo kutumia vyema fedha anazozipata kwa kujiwekea akiba na sio kuendekeza vitendo vya anasa.

"Ajira binafsi zinathaminiwa hata na serikali yenu na ndio maana shughuli mnazozifanya zinatambulika na hata uamuzi wenu wa kuanzisha chama hiki, zilipata baraka zote za serikali na ndio maana mmeandikishwa kisheria," alisema.

Mwisho alisisitiza suala la uaminifu kwa viongozi wa Chawapimbi ili kujenga imani kwa wanachama jambo ambalo litasaidia wasiojiunga kujiunga na hivyo kuongeza idadi ya wanachama ambao kwa sasa wapo 150.

Alisema kila dereva anapaswa anapaswa kuzingatia sheria zilizopo pindi anapokuwa barabarani ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikijitokeza kila siku.

No comments:

Post a Comment