03 January 2013
CHADEMA yajibu mapigo ya CCM
Na Rashid Mkwinda, Mbeya
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Mbeya, kimesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinajidanganya kinaposema jimbo hilo litarudi kwa chama tawala mwaka 2015.
Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Joseph Mbilinyi, aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Soko la SIDO,
na kusisitiza kuwa, kasoro za kiutendaji katika mfumo wa uongozi wa Serikali ya CCM, zinawafanya wananchi waendelee kukikataa chama tawala ambacho tayari kimepoteza mwelekeo.
Alisema CHADEMA kina uwezo wa kuongoza jimbo hilo kwa
zaidi ya miaka 15 ijayo kutokana na Serikali ya CCM, kuendekeza vitendo vya rushwa na ufisadi katika sekta za huduma za kijamii.
Aliongeza kuwa, CCM imeshindwa kutumia rasilimali zilizopo kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi hivyo kama CHADEMA itashika dola, Watanzania watanufaika na utajiri walionao, kukuza kipato chao, kujikomboa na umaskini.
“Hatupo hapa kuisifia Serikali ambayo inakusanya kodi za wananchi lakini wananchi wake maskini tangu uhuru hadi sasa, viongozi wa CCM wanasimama majukwaani kulumbana na CHADEMA kwa kuwaeleza wananchi mambo yasiyo na tija kwao.
“Sisi tutaendelea kuwashinikiza wananchi wakikatae chama tawala kwa kuwa hakina mtazamo wa kuboresha maisha ya Watanzania, vionmgozi wa CCM mkoani hapa wanatamba kuwa watalikomboa jimbo hili na kudai wameboresha maisha ya wananchi kauli ambayo ni dhaifu kulingana na historia ya Mkoa huui,” alisema.
Aliongeza kuwa, yeye kama mbunge wa jimbo hilo anajivunia mafanikio aliyowapa wananchi ambayo walishindwa kuyapata miaka ya nyuma.
“Siwezi kuacha kuzungumzia mafanikio ya miundombinu ya barabara tangu nilipochaguliwa ambazo zinapitika kirahisi, mbunge aliyepita hakuweza kufanya mambo kama haya,” alisema.
Alisisitiza kuwa, wananchi jimboni humo wanafahamu chama kilichosimama kidete kupigania haki zao ni CHADEMA ndio
maana wakakipa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa 2010
na wataendelea kufanya hivyo 2015.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema Serikali inapaswa kujifunza na kukiri makosa waliyofanya kwa zaidi ya miaka 50.
“Tutaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya rushwa, wizi na ufisadi unaofanywa na viongozi wa CCM, huwezi kuwalazimisha wananchi waendelee kukiamini chama tawala wakati mifumo yao mibovu inafahamika na haina tija kwa jamii,” alisema.
Hivi karibuni, Mabunge wa Jimbo la Songwe, Wilaya ya Chunya, mkoani humo, Bw. Philipo Mulugo, alisema dhamira yake ni kuhakikisha jimbo hilo linarudi CCM katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment