28 January 2013

Bao la Tegete lamvua nguo mlemavu *Domayo augua gafla, Yanga ikishinda 3-1


Na Zahoro Mlanzi

UKISTAAJABU ya Mussa utayaona ya filauni, ndivyo unavyoweza kusema baada ya shabiki aliyedaiwa kuwa wa timu ya Yanga, kuingia uwanjani huku sehemu kubwa ya mwili wake ikiwa tupu akishangilia bao la tatu lililofungwa na Jeryson Tegete katika mchezo uliopigwa Uwanja wa taifa, Dar es Salaam.

Shabiki huyo ambaye alikuwa mlemavu alistukiwa yupo nyuma ya goli la Kusini la uwanja huo akielekea kuingia ndani ya uwanja lakini kabla hajazifikia nyasi za uwanja huo, maaskari waliokuwepo uwanjani walimzuia na kumbeba kindakindaki na kumtoa nje.

Chakushangaza shabiki huyo alikuwa amebaki na nguo inayofanana na bukta tu katika mwili wake ambayo iliziba eneo la nyuma na mbele lakini sehemu kubwa ilibaki ikiwa haina nguo na kuzua maswali mengi kwa mashabiki wengine wakijiuiliza amefikaje uwanjani hapo.

Dakika tano baada ya shabiki huyo kutolewa nje, alionekana mmoja wa askari akibeba nguo za shabiki huyo zilizodaiwa kabla ya kuingia uwanjani alizivua na kitendo hicho ndicho kilichozua maswali zaidi, kwamba ilikuwaje mpaka kufika nyuma ya goli na kuvua nguo asionekane na alipoanza safari ya kuingia uwanjani ndipo aonekane.

Shabiki huyo alishindwa kujizuia kutokana na bao hilo lililofungwa na Tegete dakika ya 65, akimalizia pasi safi iliyopigwa na Nurdin Bakari aliyekimbilia mpira uliopigwa na Hamis Kiiza aliyeingia badala ya Didier Kavumbagu.

Katika mechi hiyo ya jana, Yanga iliichapa Prisons ya Mbeya kwa mabao 3-1 na kuifanya timu hiyo kuzidi kupaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo sasa imefikisha pointi 32 huku Azam ikiwa katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 na Simba pointi 26.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Jeryson Tegete katika dakika za tisa na 65 na lingine kufungwa na Mbuyu Twite katika dakika ya 57 huku la kufutia machozi la Prisons likifungwa na Misango Magai katika dakika ya 16.

Kipindi cha kwanza Yanga ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa na kufanya mashambulizi ya nguvu ambapo Prisons ilikuwa ikichezewa nusu uwanja kutokana na kila wakati kushambulia.

Pamoja na mashambulizi hayo lakini mpaka dakika 45 za kwanza zikimalizika timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili Prisons ilikuja juu na kucheza kwa kujiamini na kuliandama lango la Yanga lakini kikubwa kilichowaangusha ni safu ya ushambuliaji yao haikuwa makini katika kukwamisha  mpira wavuni.

Kutokana na hali hiyo, Yanga ilijitahidi kutumia nafasi ilizopata lakini pia itabidi wajilaumu kutokanana Tegete kukosa mabao ya wazi zaidi ya mawili katika dakika za 58 na 79 licha ya kuifungia timu yale mabao mawili.

Wakati huohuo, Kiungo chipukizi wa Yanga, Frank Domayo jana aliugua gafla kabla ya mechi hiyo kuanza na kulazimika Kocha wa timu hiyo, Ernest Brandts kumuondoa katika orodha ya wachezaji watakaoanza mechi hiyo na kumpanga Nurdin.

No comments:

Post a Comment