21 January 2013

Ajali yaua mmoja, 48 wajeruhiwa


Na Rashid Mkwinda, Mbeya

MTU mmoja amefariki dunia na wengine 48 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Nganga Express lenye namba za usajili T 413 AVU, baada ya kupinduka kwenye Mlima wa Imezu, jana asubuhi.

Basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam ambalo dereva wake, alishindwa kulimudu katika mteremko mkali kwenye eneo lenye kona wakati akiikwepa gari nyingine aina ya Fuso ili wasigongane uso kwa uso.

Wakizungumza na gazeti hili, mashuhuda wa ajali hiyo walisema kutokana na hali hiyo, dereva wa basi alilazimika kulikwepa gari gilo ndipo akapinduka.

Kwa upande wake, dereva wa basi hilo Bw. Alex Bunyinyiga, alisema baada ya kuona wanataka kugongana na Fuso, alijaribu kulipita lori lililokuwa limeegeshwa mbele yake kulia na wakati akiliweka sawa lilimshinda na kupinduka.

Abiria aliyenusurika katika ajali hiyo, Noah Elias, alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori ambalo liliharibika ambaye hakuweka alama yoyote ya tahadhari.

Alisema kama dereva wa basi hilo asingechukua uamuazi wa haraka kulikwepa Fuso, wangeweza kugongana uso kwa uso na madhara yake yangekuwa makubwa zaidi.

Muuguzi wa Zamu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Bilhuda Feruz alisema wamepokea majeruhi 48 walipokelewa hospitali hapo kati yao wanane wamelazwa lakini hali zao zinaendelea vizuri baada
ya kupatiwa matibabu.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani Athuman, alisema abiria waliokuwa wakisafiri katika basi hilo walikuwa 53 kati yao 45 walitibiwa katika hospitali hiyo na kuruhusiwa.

“Aliyefariki katika ajali hii ni Enock Lwila, mkazi wa Kitongoji cha Mama John, jijini Mbeya...marehemu alikutwa na fedha sh. milioni 13 ambazo ziliokolewa na askari waliowahi kufika eneo la tukio.

“Fedha hizi ziko salama mikononi mwa polisi na baada ya wana ndugu kujitokeza, tutazikabidhi kwao,” alisema.

No comments:

Post a Comment