21 January 2013

Waandidhi Mbeya watimua viongozi wao kwa ubadhirifuNa Rashid Mkwinda, Mbeya

UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Mbeya, umelazimishwa kujiuzulu na wanachama kutokana na tuhuma
za ubadhirifu wa fedha za klabu uliofanyika kwa miezi minne.


Hali hiyo imetokana na viongozi wa klabu hiyo akiwemo Mwenyekiti wake Christopher Nyenyembe na Mweka Hazina,
Pendo Fundisha, kudaiwa kughushi nyaraka za klabu na kutoa
fedha benki sh. milioni 44, bila idhini ya Kamati ya Kuu.

Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa dharura ulioitishwa na wanachama 41 ambao ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa UTPC Abubakar Karsan, ambapo viongozi hao walidaiwa kutoa fedha
hizo katika akaunti ya CRDB Tawi la Mbeya.

Ilidaiwa kuwam kwa nyakti tofauti viongozi hao wawili walikuwa wakienda benki kuchukua fedha wakitumia kadi ya dharura bila kuifahamisha Kamati Kuu yenye mamlaka ya kuidhinisha matumizi ya fedha ambapo hali hiyo iliibua maswali mengi kwa wanachama.

Viongozi hao walilazimika kujiuzulu baada ya Kamati Kuu ya klabu kukataa taarifa yao ya fedha mara nne iliyokuwa na kasoro ambapo walipotakiwa kuirekebisha bado ilikuwa na matatizo, baadhi ya tarakimu zikighushiwa.

Baada ya kujiuzulu nyadhifa zao na kukaa pembeni, Bw. Karsan na Mwenyekiti wa muda, Ulimboka Mwakilili walitoa utaratibu wa kuundwa kamati ya muda ya watu saba kuchunguza tuhuma hizo kwa muda wa miezi minne na baadaye kumtafuta mkaguzi wa nje ambaye atafanya ukaguzi wa nyaraka zote za utoaji wa fedha benki pamoja na matumizi yake.

Wanachama waliopendekezwa katika kamati hiyo ni Brandy Nelson (Mwenyekiti), Uswege Luhanga (Katibu), Emanuel Lengwa (Mweka Hazina) na wajumbe wanne ambao ni Esther Macha,
Festo Sikagonamo, Modest Nkulu na Hosea Cheyo.

Awali ilidaiwa katika mkutano huo kuwa, viongozi hao walikuwa wanaghushi risiti za mtu aliyepangwa kuhudumia wanahabari wanaoshiriki semina ambapo zaidi ya sh. milioni 10, zinadaiwa kutumika katika semina tisa.

1 comment: