03 January 2013

Risasi 7,640, silaha 57 zakamatwa Kigoma





Na Mwajabu Kigaza, Kigoma

JESHI la Polisi mkoani Kigoma, limefanikiwa kukamata risasi
7,640, silaha 57, mabomu manane ya kutupa kwa mkono pamoja
na watuhumiwa 36 wanaojihusisha na mauaji ya kutumia silaha katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2012.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fraisser Kashai, alisema kukamatwa kwa silaha hizi kumetokana na ushirikiano mzuri
uliooneshwa na wananchi kwa jeshi hilo.

Alisema kati ya silaha zilizokamatwa ni pamoja na SMG 32,
Short gun tatu na gobore 22, ambazo zilikuwa zikitumika katika matukio mbalimbali ya kuteka magari ya abiria, kufanya mauaji
kwa wananchi pamoja na uhalifu katika hifadhi.

Aliongeza kuwa, watuhumiwa 36 walikamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo kati ya hao Watanzania 29 na raia wa nchi jirani ya Burundi saba.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limeshiriki kikamilifu katika ufungaji wa kambi ya Wakimbizi ya Mtabila kwa kushirikiana
na vyombo vya ulinzi vya Wilaya, Mkoa, Idara za Serikali na
zisizo za Serikali kwa kuhakikisha wakimbizi wote wanarejea
nchini kwao kwa usalama.

Alisema wakimbizi 34,0919 wamerudishwa nchini Burundi kwa amani ambapo kutokana na hali ya kijiografia ya Mkoa huo, jeshi
hilo limeendelea kuanzisha Vituo vya Polisi ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati.

No comments:

Post a Comment