03 December 2012

Ziwa Rukwa sasa hatarini kukauka



Na Rashid Mkwinda, Momba

HALI ya viumbe hai katika Ziwa Rukwa, lililopo pembezoni mwa Kata za Ivuna, Mpapa na Kamsamba, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya, zipo hatarini baada ya ziwa hilo kujaa tope kutokana na
mito inayoingiza maji ziwani kukauka.

Mizigo ya baadhi ya viumbe ambavyo maisha yao hutegemea maji ya ziwa imeanza kuonekana ambapo ndege weupe, nyange nyange, bata mzinga na vonga vonga, wameanza kutoweka na kusababisha wafugaji kutumia ziwa hilo kulishia ng’ombe wao.

Kundi la ng’ombe wanaokadiriwa kufikia 300,000 wamegeuza eneo hilo kuwa sehemu ya malisho na kusababisha uharibifu wa mazigira ambapo baadhi ya wakazi waishio maeneo ya pembezoni mwa ziwa wanaendelea na shughuli za kilimo.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, walisema idadi kubwa ya mifugo ya wafugaji waliohamishwa katika ardhi oevu ya Ihefu, wilayani Mbarali, imevamia ziwa hilo wakitokea wilayani Chunya.

“Kabla ya uvamizi huu, miaka ya nyuma ziwa hili lilikuwa linavutia, kulikuwa na viboko, mamba lakini hivi wamekimbia, hata samaki wamepungua, unaweza kukaa mwezi mzima bila kuambulia kitoweo cha samakiw,” alisema Elivathan Silwimba, Ofisa Uvuvi Kata ya Ivuna.

Alisema uharibifu huo wa mazingira umechagia kukausha Mto Mombo ambao unaingiza maji katika ziwa hilo ukikusanya maji katika mito mingine iliyopo wilayani Mbozi ambapo Mto Songwe unaingiza moja kwa moja ziwani pamoja na Mto Nkana.

Aliongeza kuwa, shughuli za kilimo zinazoendelea ndani ya hifadhi ya ziwa hilo, zimesababisha madhara kwa mazalia ya samaki na viumbe hai waishio ufukweni, kulifanya ziwa kujaa tope na kupoteza mandhari yake halisi na kutoweka kwa ndege adimu.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbozi, Joel Kaminyoge, alisema njia pekee inayoweza kusaidia kuokoa ardhi hiyo ni kupunguza idadi ya mifugo kwa wanakaya kwani wanachangia kuondosha uoto wa asili pembezoni mwa ziwa.

Alisema kuwa ng’ombe mmoja ana uwezo wa kunywa zaidi ya lita 40 kwa mkupuo ambapo idadi ya ng’ombe 300,000 wanaoingia ziwani kwa siku wankunywa takribani lita milioni 12.

“Ukichanganya na uharibifu mwingine wa ujenzi na kilimo unaoendelea katika vyanzo vya maji maeneo ya Ikonongo na Nyimbili wilayani hapa, ziwa lazima likauke,” alisema.

Kaimu Ofisa Wanyamapori wilayani humo, Charles Ndimbwa, alisema kutoweka kwa wanyama katika ziwa hilo kumechangiwa
na uharibifu wa mazingira unaotokana na ufugaji holela pamoja na wafugaji kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe.

No comments:

Post a Comment