03 December 2012
Walimu waidai serikali bil. 24/-
Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hadi sasa kinaidai Serikali sh. bilioni 24 ambazo ni malimbikizo ya madeni ya walimu 45,000.
Katibu Mkuu wa CWT, Bw. Ezekiel Oluoch, aliyasema hayo mjini Kibaha, mkoani Pwani jana wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akikabidhi jengo la chama hicho wilayani humo na kuongeza kuwa kati ya fedha hizo sh. milioni 200 ni za walimu
wa shule za msingi.
Alisema mbali ya fedha hizo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kupitia idara inayosimamia wakaguzi wa shule na wakufunzi, bado haijawalipa wakufunzi na wakaguzi
sh. bilioni 1.5.
“Wakaguzi wa shule ngazi ya Wilaya nchini wapo 700 na wakufunzi 12,700, lakini hadi sasa tunashangaa kwanini Serikali imeshindwa kupunguza deni hili au kulimaliza kabisa wakati Hazina ilishalipa sh. bilioni 3.5 mwishoni mwa 2011,” alisema Bw. Oluoch.
Aliongeza kuwa, Serikali inapaswa kuepuka migogoro isiyo ya lazima ambayo kwa kiasi kikubwa inashawishi kufanyika migomo inayokwamisha maendeleo ya nchi.
Akizungumzia muafaka kati ya chama hicho na Serikali, Bw. Oluoch alisema hakuna mgomo uliositishwa na Mahakama Kuu ambapo CWT ilikata rufaa Oktoba 25 mwaka huu na hivi sasa
rufaa yao inasubiri kupangiwa jaji wa kuisikiliza.
“Tumetuma maombi kwa Serikali iunde tume ya watu wachache ambao tutakaa nao meza moja na uongozi wa CWT Taifa ili tuweze kufikia muafaka,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment