04 December 2012

Wawili wafariki, 16 wajeruhiwa


Zubeda Mazunde na Angelina Faustine

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya magari matatu kugongana katika eneo la Kibamba Shule, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema ajali hiyo imetokea juzi saa 2:30 katika eneo hilo.

Alisema ajali hiyo imuhusisha gari yenye namba za usajili T 247 AAV, aina ya Toyota Hilux iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika akitokea Kibwegere.

Kamanda Kenyela alise,a gari hilo liliacha njia na kuingia katika barabara ya Morogoro ambapo gari yenye namba za usajili T 617 BQX, iliyokuwa upande huo, ilihama upande wa pili na kwenda kugongana na gari yanye namba za usajili T 629 ATK.

Alisema abiria wa gari yenye namba T 629 ATK, walifariki dunia papo hapo ambao ni Hamis Hiyana (35), mkazi wa Kibaha na mwanaume mmoja asiyefahamika ambaye anakadiriwa kuwa
na umri wa miaka (35-40).

“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha na majeruhi walipelekwa hospitalini hapo kwa matibabu zaidi,” alisema.

Wakati huo huo, Aisha Amiri (35), mkazi wa Jangwani anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya kete 14.

Kamanda Kenyela alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi
saa 4 asubuhi, eneo la Kariakoo wakati polisi wakiwa doria.

No comments:

Post a Comment