13 December 2012
Wavunja ofisi, kumuua mtuhumiwa
Na Faida Muyomba, Geita
BAADHI ya wakazi wa Kijiji cha Bwera, Wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, wamemuua Habibu Daudi (30), kwa kipigo baada
ya kuvunja Ofisi ya Mtendaji Kata alipokuwa amehifadhiwa kwa tuhuma za wizi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Leonard Paulo, alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni kijijini hapo baada ya mtuhumiwa kuiba bati sita.
Alisema marehemu alikamatwa na kundi la watu katika Kijiji cha Kasosobe na kumpeleka kwenye Ofisi ya Mtendaji Kata ya Mbogwe lakini baadaye walivunja mlango na kuanza kumpiga kwa mawe na virungu hadi kifo chake.
Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi dhidi ya tukio hilo ambapo hadi sasa hakuna mtu yoyote anayeshikiliwa na kutoa
onyo kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapa adhabu watuhumiwa.
Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Katale, Wilaya ya Chato, mkoani humo, Esther Emmanuel (30) amekufa baada ya kupigwa
na radi.
Kamanda Paulo alisema, tukio hilo lilitokea Desemba 10 mwaka huu, saa tisa alasiri wakati marehemu akiwa nyumbani kwake na nyumba yake ya nyasi imeharibiwa vibaya kutokana na radi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment