13 December 2012

Walanguzi nauli Ubungo kusakwa *SUMATRA yaaanza msako mkali



 Na Grace Ndossa

MAMLAKA ya Udhibiti, Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imeanza ukaguzi wa mabasi yaendayo mikoani yanayotoza nauli kubwa kwa abiria katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, Dar es SAlaam (UBT).

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA, Kanda ya Mashariki, Konradi Shio, alisema ukaguzi huo ulinza jana saa 11 alfajiri.

Alisema baadhi ya mabasi huwa na kawaida ya kupandisha nauli kinyemela katika msimu huu wa sikukuu na kusababisha kero kwa abiria.

“Operesheni hii itaendelea hadi msimu wa sikukuu umalizike kwani madereva wengi hupandisha nauli ili waweze kupata fedha nyingi na kusababisha abiria kupata shida,” alisema Shio.

Aliongeza kuwa, SUMATRA imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa abiria mara kwa mara kutokana na kupandishiwa nauli hivyo wengi wao hushindwa kusafiri kutokana na nauli kuwa kubwa.

Alisema tangu waaanza kukagua mabasi hayo, mengi yameonekana kutoza kiwango kinachotakiwa lakini kama wasipokuwepo vituoni, mabasi mengi hupandisha nauli bila woga.

Aliwataka wamilikia wa mabasi, kuwaonya mawakala wao ili waache kutoza  nauli kubwa tofauti na iliyopangwa.


No comments:

Post a Comment