27 December 2012

Wasra ataka kuundwa kamati za shule Bunda



Na Raphael Okello,Bunda.

WAZIRI wa nchi Ofisi ya rais Mahusiano na uratibu Stephen Wasira amewataka wazazi kuunda kamati na bodi za shule ili kusimamia michango na maendeleo ya shule badala ya kuwaachia wakuu wa shule pekee.

Akijibu kero za wananchi jimboni mwake jana katika vijiji mbalimbali, Wasira ambaye ni mbunge wa jimbo la Bunda alisema michango mingi ni kutokana na wakuu wa shule kufanya maamuzi wao wenyewe.

Aliwataka maofisa elimu katika  halmashauri kusimamia uundaji wa kamati za wazazi kwa kila shule za msingi na bodi za sekondari ili ziweze kutathmini maendeleo na kero mbalimbali kati ya wazazi, wanafunzi na walimu.

“tatizo ni kwamba wazazi mmewaachia wakuu wa shule kujiamulia kila kitu kuhusu shule, kwa mfano, michango ya madawati kila mwaka, hivi madawati hayo yanaenda wapi, Kamati na bodi  za wazazi zinapaswa kujua” alisema Wasira.

Awali wazazi na walezi  walimwambia Wasira kuwa wanashangazwa na michango shuleni kila mara wakati ambapo serikali ilitoa agizo kuwa michango mingi isiyolazima wasitoe wazazi.

Suala la michango ya madawati kila mwaka, majembe, ndoo na vifaa vingine viliwekera wazazi  huku wakihoji kuwa hata vile vinavyodaiwa kuharibika havionekani shuleni.

No comments:

Post a Comment