03 December 2012
Wananchi 903 kukosa makazi Dar *Serikali yatoa tamko la mgogoro wao
Na Rachel Balama
SERIKALI imewataka wananchi 903 wenye mgogoro wa ardhi eneo la viwanja namba moja, nne na saba, linalomilikiwa na Kiwanda cha Saruji Wazo Hill, kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam, kuondoka kwani walivamia eneo hilo hivyo hawastahili kuwepo.
Msimamo huo umetangazwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, wakati akizungumza katika mkutano maalumu uliohusisha viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa wananchi hao ili kutoa msimamo wa Serikali kuhusu sakata hilo.
Alisema watu hao wanatakiwa kuhama kwani Serikali inatekeleza agizo la Mahakama ya Rufaa ambayo tayari ilitoa humuku kuwa eneo hilo ni mali ya kiwanda hicho hivyo Serikali inapaswa kuwatafutia eneo ili waondoke.
“Serikali itawajibika tuwatafutie eneo kama ilivyoariwa na mahakama,” alisema Prof. Tibaijuka na kuongeza kuwa, kuanzia wiki ijayo wataenda kupima mipaka ya eneo husika na kutuma mtathmini ambapo hatua hizo zinapaswa kukamilika ndani ya
mwezi mmoja.
Alisema eneo ambalo watapewa wananchi hao, lilikuwa limepatikana Mabwepande, lakini baada ya kutokea
mafuriko, eneo hilo walipewa wakazi wa mabondeni.
Aliwataka wananchi hao, kukubali eneo hilo lipimwe, kufanyiwa tathmini ili waendelee na taratibu zingine pamoja na kuwatafutia eneo.
Prof. Tibaijuka aliongeza kuwa, ili kuuondokana na migogoro
kama hiyo Wizara ya Nishati na Madini itaorodhesha malighafi
zote zilizopo eneo husika na mameneo yaliyo karibu ya kiwanda
hicho ili nayo yatwaliwe.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wake, Diwani wa Kata ya Wazo Hill, Bw. John Moro, alimuomba Prof. Tibaijuka, azungumze na Rais Kajaya Kikwete ili awaruhusu wananchi hao waendelee kuishi eneo hilo na hati ya kiwanda ifutwe ili wasiweze haki zao.
Alisema kama Rais atakataa ombi hilo, tathmini ifanyike na wananchi walipwe gharama zao kulingana na sheria ya sasa
kama watakavyolipwa wakazi wa Kigamboni.
Mkazi wa Chasimba, Kudra Ally alisema hakuridhishwa na uamuzi wa Serikali pamoja na Mahakama kwani wao wanaishi katika eneo hilo kihalali.
“Vielelezo vyote tunavyo hivyo eneo hili si la kiwanda bali kuna mchezo mchafu unaofanywa kati ya Serikali na uongozi wa kiwanda ndio maana tunalazimishwa kuondoka,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment