03 December 2012

Waliomwibia 'Sharo Milionea' wasalimisha vitu vyake



Na Mashaka Mhando, Tanga

WATU wanaodaiwa kuiba vitu mbalimbali vya marehemu Hussein Mkieti 'Sharo Milionea', aliyefariki Novemba 26 mwaka huu, kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Songa Kibaoni, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wamesalimisha baadhi ya vitu walivyoiba kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho na kuendelea kuishi mafichoni
wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi.


Kusalimishwa kwa vitu hivyo kumetokana na agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Subira Mgalu, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama, kudai watu wote waliomwibia marehemu baada ya ajali, watasakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani kitendo walichokifanya si cha kiungwana.

Kutokana na kitendo kilichofanywa na watu hao, Jeshi la Polisi wilayani humo, juzi usiku lilifanya msako mkali lakini halikuweza kuwakuta baadhi ya watu katika nyumba zao ambao walilazimika kuhama makazi yao wakiogopa kukamatwa.

Polisi hao walizitaka familia walizozikuta katika nyumba hizo kutoa ushirikiano ili watu waliohusika na wizi huo waweze kukamatwa na kurudisha vitu hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, ACP Constatine Masawe, alisema usiku wa kuamkia jana Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. Abdi Zawadi, alipelekewa vifaa mbalimbali ikiwemo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa pamoja na spea ya tairi ambalo waliling'oa na kutokomea nalo.

Alivitaja vitu vilivyokabidhiwa kuwa ni begi la marehemu ambalo lilikuwa na nguo zake, betri ya gari hilo lililokuwa na namba za usajili T 478 BVR, aina ya Toyota Harrier, saa yake ya mkononi, simu yake aina ya Blackberry na redio ya gari ambayo iling'olewa.

“Vitu hibvi vilipelekwa na mtu mmoja ambaye kwa sasa hatuwezi kumtaja jina lake kwani alijitambulisha kuwa an undugu na wezi ambao walimpa vitu hivyo avipeleke kwa uongozi wa kijiji hivyo tunafanya uchunguzi ili kuwatia nguvuni wote waliohusika.

“Tuliweka mtego baada ya kusikia kuna mwizi mmoja anatafuta mteja wa simu ya mkononi aliyokuwa akiitumia marehemu lakini kijana huyo wakati akijadiliana bei na mtu tuliyemuweka, alibaini
na alipompa simu hiyo mkononi alikimbia vichakani ili asiweze kukamatwa,” alisema Kamanda Masawe.

No comments:

Post a Comment