03 December 2012
Ubunge wa Mnyika sasa wakatiwa rufaa *Pingamizi kusikilizwa na jopo la Majaji watatu
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Rufaa jijini Dar es Salaam, Desemba 7 mwaka huu inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa ya kesi ya uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ubungo.
Rufaa hiyo imefunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa
jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Hawa Ng'humbi dhidi ya Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Jopo la Majaji watatu ndio litakalosikiliza rufaa hiyo akiwemo Natharia Kimaro, Salum Massati na Catherine Oriyo.
Bi. Ng'humbi amekata rufaa hiyo akipinga hukumu iliyotolewa
na Jaji Upendo Msuya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam iliyompa ushindi Bw. Mnyika.
Katika hukumu yake, Jaji Msuya alisema Mahakama hiyo imetupilia mbali madai yote ya mlalamikaji Bi. Ngh'umbi kwa sababu ushahidi aliouwasilisha ulijikita katika ushahidi wa kusikia ambao mahakama kamwe haiwezi kuupokea.
Alisema Mahakama hiyo kwa kauli moja inamtangaza Bw. Mnyika kuwa mbunge halali wa Jimbo la Ubungo na kwamba taratibu zote za uchaguzi zilifuatwa.
Katika kesi hiyo, Bi. Ng'humbi eliyekuwa akitetewa na wakili Bw. Issa Maige, alikuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yaliyompa ushindi Bw. Mnyika.
Bi. Ng'humbi katika hati yake ya madai namba 107/2010, pamoja na mambo mengine aliiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi wa Jimbo la Ubungo ulikuwa batiri kwa sababu haukuwa huru na haki ambapo taratibu za uchaguzi zilikiukwa.
Alidai Bw. Mnyika aliingiza kompyuta ndogo (Laptop), kwenye chumba cha kuhesabia kura, kuzitumia kwa kujiongezea kula na kumtolea maneno ya kashfa wakati wa kampeni za uchaguzi kwa kumuita fisadi alipokuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (CWT) Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment