19 December 2012

Waiomba serikali imbane mwekezaji arudishe ardhi



Na John Gagarini, Bagamoyo

WAKAZI wa Kijiji cha Changarikwa, Kata ya Mbwewe, Wilaya
ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wameiomba Serikali kuingilia kati
utata uliopo kati yao na mwekezaji aliyepewa eneo la ekari 500
ili waweze kurudishiwa baada ya kushindwa kuliendeleza.


Msimamo huo umetolewa mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo ambao uliandaliwa na Jumuiya ya Waazi ya CCM wilayani humo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Bw. Abdul Sharifu.

Mkazi wa kijiji hicho, Bw. Juma Mohamed, alisema kwa muda mrefu tangu mwekezaji apewe eneo hilo, ameshindwa kufanya
jambo lolote la maendeleo pamoja na kulifanyia usafi.

“Tunaiomba Serikali itusidie ili eneo hili liweze kurejeshwa katika Serikali ya kijiji na kutumika kwa huduma za jamii badala ya kuendelea kubaki kwa mwekezaji,” alisema.

Alisema mbali ya mwekezaji kushindwa kuliendeleza eneo hilo, ahadi aliyoitoa wakati akiliomba ya kujenga zahanati na kutoa
trekta nayo ameshindwa kuitekeleza.

“Huyu mwekezaji aliomba kupewa eneo hili ili afanye shughuli za kilimo ambazo zitakinufaisha kijiji chetu lakini ameshindwa kufanya hivyo sasa tunalihitaji eneo letu,” alisema Bw. Mohamed.


Kwa upande wake, diwani wa Kata ya Mbwewe, Bw. Omary Mhando, alisema mwekezaji huyo alipewa eneo hilo mwaka 2003 na walijaribu kuwasiliana naye ili waweze kujua sababu zilizomfanya ashindwe kuliendeleza lakini hawajampata.

“Miaka mitatu imepita mwekezaji hajaonekana hapa kijijini, ili wananchi waweze kurudishiwa eneo hili wanapaswa kuandaa mkutano na kupitisha azimio la kutka eneo lao, taarifa za mkutano huo zitapelekwa halmashauri kwa hatua zaidi,” alisema.

No comments:

Post a Comment