21 December 2012

Wahariri: Tunataka uhuru wa vyombo vya habari



Na Agnes Mwaijega

JUKWAA la Wahariri nchini (TEF), limeitaka Serikali kuhakikisha Katiba Mpya inayoandaliwa inakuwa na ibara maalumu ambayo itatoa uhuru wa vyombo vya habari nchini.


Katibu wa jukwaa hilo, Bw. Neville Meena, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maazimio mbalimbali yaliyofikiwa kwenye mkutano wa TEF, uliofanyika mkoani Tanga, hivi karibuni.

Alisema katiba inayotumika sasa ya mwaka 1977, haina kifungu chochote ambacho kinatamka uhuru wa vyombo vya habari.

Bw. Meena alisema, TEF imesikitishwa na kitendo cha katiba hiyo kutotambua uhuru wa vyombo vya habari hata baada ya kufanyiwa mabadiliko ya 14 mwaka 2005.

“Jukwaa limeipitia katiba hii kwa umakini mkubwa na kubaini hakuna neno wala kifungu kinachotoa uhuru wa vyombo vya habari hivyo kwa masilahi ya tanisia hii na maendeleo ya nchi, tunataka kuona katiba ijayo inatamka uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa masilahi ya maendeleo ya Taifa hili, Wahariri wanataka Katiba Mpya iwe na kifungu kinachotoa haki ya kupata habari kwa wananchi wote bila kubaguliwa na kuwekewa vikwazo.

Kwa mujibu wa Bw. Meena, TEF linaitaka Serikali kukubali kutunga sheria ya huduma kwa vyombo vya habari ambayo mapendekezo yake tayari yameshatolewa na wadau wa
habari ambao wameiwasilisha serikalini.

“Wahariri kwa kauli moja tunasisitiza kuwa, nia yetu ni kuhakikisha tunashirikiana na Serikali kufanya kazi kwa weledi kwa masilahi ya Taifa na maendeleo ya nchi yetu na wati wake,” alisema.

Alisema pamoja na maazimio hayo,TEF itaratibu maoni ya Wahariri, waandishi na kuyawasilisha kwenye tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya ili kuhakikisha michango ya sekta ya habari inazingatiwa katika katiba hiyo.

Akizungumzia vyuo vya uandishi wa habari, Bw. Meena TEF imeazimia vyuo hivyo vinapaswa kuanza kutumia mtaala mmoja ulioandaliwa na NACTE,Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari. 

“Baada ya miezi sita tutafanya utafiti ili kuvibaini vyuo ambavyo vitakuwa vimekidhi matakwa ya kitaaluma, tumekubaliana kuwa, hatutapokea wanafunzi wake kwa mafunzo ya vitendo,” alisema.

Alisisitiza kuwa, vipo baadhi ya vyuo ambavyo vimekuwa vikichanganya mafunzo ya uandishi wa habari na kozi
nyingine ambazo hazina uhusiano na taaluma hiyo.

Aliongeza kuwa, maazimio mengine ni pamoja na vyombo vya habari kuzingatia maadili, kanuni, miongozo ya kitaaluma na kuepuka kuwa vyanzo vya migogoro baina ya watu, dini,
vyama vya siasa, makabila au taasisi zozote  za kijamii.

Maengine ni vyombo vya habari kuwajengea uwezo waandishi chipukizi, kuwashauri wamiliki wa vyombo husika kuzingatia vigezo vya kitaaluma pale wanapotoa ajira.

Kwa upande wa vituo vya redio na televisheni, TEF imeazimia kurekebisha vipindi vya usomaji wa magazeti kwa kuwataka mameneja wa vipindi kuacha kusoma habari zote badala yake wafanye udondozi.

“Hii inaharibu soko la magazeti nchini, kwa sababu mtu akishasikiliza kipindi cha magazeti, hawezi kwenda
kulinunua mtaani aatakuwa ameshiba kila kitu,” alisema.

1 comment:

  1. NI KWELI MUNATAKA UHURU LAKINI MASLAHI YA TAIFA YAZINGATIWE NI VIGUMU SANA KUMWANGALIA MTU USONI NA KUMTUHUMU KUWA FISADI BILA KUFUATILIA MATENDO YAKE,KADHALIKA NI VIGUMU SANA KUMTMBUA KUWA MWANDISHI WA HABARI SI MZALENDO,MAMLUKI,KIBARAKA WA WAKOLONI NA MABEBERU BILA KUFUATILIA MAKALA ZAKE KWA WAMAREKANI MIKHAIL GORBACHEV NI SHUJAA KWANI AMEWASAIDIA KUISAMBARATISHA USSR ILA KWA RUSSIA NI KIBARAKA NA LAITI NYENDO ZAKE ZINGEDHIBITIWA HALI SIASA UCHUMI ISINGEKUWA KAMA ILIVYO LEO NI VEMA SERIKALI KWA KUTUMIA USALAMA WA TAIFA WACHUNGUZE HAYO MADAI IWAPO NI KWA MANUFAA YA NCHI

    ReplyDelete