21 December 2012

CHADEMA kwachafuka *Sakata la Dkt. Slaa kumiliki kadi lazua jipya *Katibu BAVICHA adai yupo tayari kufukuzwa


Na Benedict Kaguo

HALI ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Tanga, imezidi kuwa tete baada ya Katibu wa Baraza la Vijana wa chama hicho, Bw. Deogratius Kisandu kudai Mwenyekiti wa chama mkoani humo, Bw. Saidi Mbweto, anatumika na viongozi wa CCM kuhujumu chama.

Hatua hiyo inatokana na mgogoro mkubwa ulioibuka ndani ya chama hicho mkoani humo baada ya Bw. Mbweto kumtuhumu Bw. Kisandu kwa kauli yake ya kutaka matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2010, yafutwe kwani CCM ilisimamisha wagombea wawili katika nafasi ya urais.

Madai ya Bw. Kisandu kutaka matokeo hayo yafutwe ni baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa, kukiri kumiliki kadi ya CCM hivyo wakati akigombea urais mwaka 2010, bado alikuwa mwanachama wa chama tawala.

Alisema kutokana na hali hiyo ni wazi kuwa CCM ilisimamisha wagombea wawili wa nafasi ya urais ambao ni Dkt. Slaa na Rais
Jakaya Kikwete ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi huo.

Akizungumza na Majira jana, Bw. Kisandu alisema yuko tayari kufukuzwa CHADEMA kama ataonekana hana nidhamu kwa kusimama kwenye ukweli.

Alisema kitendo cha kutangaza dhamira yake ya kutaka kugombea urais mwaka 2015, imekuwa mwiba kwa wanasiasa wa chama hicho pamoja na kutumika baadhi ya makundi ili kumdhoofisha kisiasa.

“Mimi siishi kwa kubembeleza cheo, dhamira yangu ya kugombea urais najua inamuumiza moyo Bw. Mbweto ndio maana anatumika kuniharibia jina kwani ni mpango wa Mungu mimi kuwa Rais wa Tanzania, mbinu anazotumia dhidi yangu hazitafanikiwa na wanaosema msaliti wo ndio wasaliti wakubwa,” alisema.

Alisema chama hicho kipo kwenye mgogoro mkubwa na kuhadhirisha kama hatua hazitachukuliwa, kitasambaratika kama ilivyotokea katika vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo vilipata nguvu kubwa baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi.

“Hata Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Bw. John Heche naye anipigia simu na kunilaumu kwa kauli yangu ambayo kimsingi nilitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ibadili matokeo ya uchaguzi wa urais 2010.

“CCM ilisimamisha wagombea wawili kwa mujibu wa tamko la Bw. Nape Nnauye (Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi-CCM), naamini uchaguzi wa urais ukirudiwa, CHADEMA tutashinda,” alisema.

Juzi Bw. Mbweto akizungumza na waandishi wa habari, aliweka wazi msimamo wa kupeleka mapendekezo ya kuchukuliwa hatua kali kwa Bw. Kisandu kwa kutoa kauli za kutaka Dkt. Slaa
ajiuzulu kwa kumiliki kadi ya CCM.

Wakati huo huo, Mwandishi Wilhelm Mulinda, anaripoti kutoka Mwanza kuwa, siku moja baada ya aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, Jimbo la Sumve mkoani humo, katika Uchaguzi Mkuu 2010, Bw. Milton Lutabana kujiunga CCM, jana alitoa sh. 2,400 ili kumlipia Dkt. Slaa ada ya uanachama miaka miwili hadi 2015, kwa kuendelea kumiliki kadi ya chama tawala.

Bw. Lutabana alimkabidhi fedha hizo Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Bara, Bw. Mwigulu Nchemba ili amkabidhi Bw. Nnauye
na kuziwasilisha katika tawi la chama hicho wilayini Karatu,
mkoani Arusha, ambako Dkt. Slaa aliingia uanachama.

Ada hiyo ilitolewa katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya llemela, mkoani humo, ambapo Bw. Mwigulu ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Bw. Lutabana amekuwa mwanachama wa kwanza CCM kumlipia ada Dkt. Slaa tangu, Bw. Nnauye aliposema Katibu huyo wa CHADEMA anamiliki kadi ya chama tawala na yeye mwenyewe
kukiri kumiliki kadi hiyo ambapo katika kikao hicho, wanachama 85 wa CHADEMA walihamia CCM

2 comments:

  1. TUACHE TOFAUTE ZETU KADI ISITUTENGANISHE SISI NA CHADEMA DAMU TUMETUMIA MUDA MWIGI KUKITUMIKIA CHAMA TUACHE JAZIBA

    ReplyDelete