17 December 2012

Visiwa vya Sengerema vyatelekezwa na Serikali *Hakuna zahanati wala maji safi *Kikongwe ajitosa kuokoa roho za wajawazito


Na Mobini Sarya

WAKATI  Tanzania ikisherehekea miaka 51 ya uhuru ,wakazi wa visiwa vya Sengerema, Mkoa wa Mwanza wapo katika giza baada ya serikali kutelekeza visiwa hivyo tangu uhuru.

Visiwa hivyo ni Soswa/Chembaya, Nyamango Chamagati, Kasalazi na Gembale, Yozwa na Busenge ambavyo vinahesabiwa kuwa vipo kijiji cha Lushamba Kata ya Bulyaheke jimbo la Buchosa.
 
Wakazi hao wameliambia shirika la habari (Tanpress) kwamba hawana cha kujivunia tangu nchi imepata uhuru zaidi ya kushurutishwa na serikali ya Tanzania kulipa kodi na michango mingine bila kupewa maendeleo yoyote.

“Kama unavyoona mwandishi katika eneo hili ambalo lina visiwa vinne vyenye kuundwa na vitongoji viwili hatujawahi kuletewa huduma muhimu kama wanazopata watanzania wengine, ”anasema George Rwezaula Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyamango na Chamagati.

Hivi ni visiwa viwili tafauti lakini kwa makusudi serikali imeviacha kuwa kitongoji kimoja chanye wakazi  zaidi ya 3500 na kaya 75 wakati kitongoji kinatakiwa kisizidi kaya 50, pia kuna visiwa zaidi ya 7 eneo hilo ambavyo vilipaswa kuundiwa kijiji ili kusogeza huduma karibu.

Anasema kuwa visiwa hivyo vina ukosefu wa huduma muhimu za kijamii ikiwemo vituo vya afya, shule, maji safi na kituo cha polisi.

Akizungumza na TanPress katika kisiwa cha Nyamango , Rwezaula alishukuru kutembelewa na Mwandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu historia ya uhuru jambo lililosababisha kuchelewa kwa maendeleo eneo hilo.

“Mwandishi kwanza tunakushukru kuweza kufika katika kisiwa chetu, hakuna mwandishi ambaye amewahi kuja hapa, licha ya kwamba kuna matukio makubwa  na kutisha  ambayo hufaanyika hapa kama ujambazi wa kutisha lakini taarifa hazifiki kwenye vyombo vya habari,”anasema.

Anasema, hakuna kituo cha Polisi, kati ya Mwezi Septemba hadi Novemba Mwaka huu wavuvi visiwa hivyo waliporwa zaidi ya mashine 100 za mitumbwi na maharamia usiku, lakini walipotoa taarifa, jeshi la polisi ilichukua siku tano kufika kwenye tukio.

“Hatuna huduma ya Polisi ndio maana majambazi huingia kila wakati kwasababu kituo kinachotuhudimia kipo nchi kavu kilomita 60, ukiwapigia simu polisi wanasema hawana mafuta hadi wachangishane,” anasema.

Kamanda Polisi Mkoa wa Mwanza anasema “Wambie wananchi wapeleke malalamiko yao Halmashauri…mbona  wanalipa kodi kwanini wasijegewe vituo kama njia ya kuletewa maendeleo  ……ujue mazingira yao ni tofauti unakuta kisiwa kina watu wachache labda wabuni njia nyingine ya kujilinda kama ulinzi shirikishi kwasababu usafiri kwenda kwao ni taabu ….mazingira yao ni magumu,” anasema RPC Erenest  Mangu.

Anaongeza kuwa vituo vyote ni mali ya jamii “Wakijenga tu hata kesho ungewashauri wajenge kituo cha poli sisi tuwapelekee askari,………kama magari yenyewe ni taabu kufanyia doria nchi kavu, usafiri wa boti tutapataje kufika visiwa hivyo? Tutawapelekea askari kama wakijenga vituo……..,wabunge wa maeneo yao wangekuwa wanapiga kelele za namna hiyo hata magari na usafiri wa boti ungekuwa umepatikana," anasema Mangu.

Licha ya visiwa hivyo kuwa maili 45 kutoka jijini Mwanza na Kilometa 120 kutoka wilayani Sengerema havina huduma yoyote ya afya wala usafiri wa uhakika kuweza kuwafikisha wagonjwa na wajawazito kwenye kituo cha afya.

Kukosekana kwa kituo cha afya wala zahanati karibu kumesababisha ongezeko la vifo vya akinama wajawazito licha ya kwamba kila mwaka serikali hutenga bajeti ya afya iliyopaswa kugawanywa katika maeneo yote.

Mwandishi wa makala alilazimika kukodi usafiri na kutembea kutwa kwenye visiwa saba kutafuta huduma ya kituo cha afya hakuweza kukipata badala yake aliambiwa aende nchi kavu ilipo zahanati ya kijiji kilometa 40 ambapo hata hivyo baada ya kufika alikuta imefungwa kwa maelezo kuwa jumapili hakuna huduma inayotolewa.
 
Akizungumza kwenye kibanda chake cha kuuzia dawa Mganga muuguzi wa zahanati hiyo, Yasinta Midale anasema kuwa licha ya kuwa tegemeo kubwa kwa wakazi wa visiwani lakini haina huduma mhimu.

“Kwamfano hapa tuna muda mrefu hatupimi maambukizi ya VVU kwa akina mama wajawazito kwasababu hakuna vipimo hata vya malaria hivyo ingawa tunapokea wajawazito 78 hadi 85 kwa mwezi wanahitaji huduma ya kliniki ,” anasema.

Kukosekana kwa huduma ya afya kumemsukuma kikongwe mwenye miaka 55 kuanza shughuli ya ukunga katika visiwa vinavyomzunguka.

Mama Madewa anasema, alianza huduma hiyo mwaka 2007 baada ya kuona serikali imeshindwa kuwasaidia akinamama wanateseka na kupoteza maisha.

“Wakati huo akinamama walipokuwa wanaona wamekaribia kujifungua walikuwa wanasafiri kwenda nchi kavu kusubiria, lakini kuna wale ambao waliendelea kutafuta pesa na kukuta muda wakujifungua umefika hao ndio walikuwa wanapata taabu hadi nilipoanza hii kazi,” anasema Bi.Madewa

Licha ya kuhudumia akimama wa visiwa vya Chamagati, Nyamango, Chembaya na zilagula vyenye wakazi zaidi ya 10000 bado serikali haijawahi kumpatia mafunzo yoyote hata ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyamango, amedai kwamba mara kadhaa aliwahi kupeleka ombi la mkunga huyo kwenye vikao vya kata ili apatiwe  mafunzo lakini serikali ya wilaya ilidai kuwa bajeti imefika kikomo.

"Nashangaa serikali kupitia Mamlaka ya mapato TRA kufika hapo mara kwa mara kukusanya kodi, halmashauri nayo kukusanya ushuru lukuki lakini  wameshindwa kupewa huduma yoyote ya kijamii ikiwemo maji safi,".

Ametaja baadhi ya ushuru unaokusanywa na serikali kuwa ni shilingi 90,000 za kusajili mtumbwi kwa namba MSR, leseni kila mwaka 35000 huku mitumbwi kwenye kisiwa kimoja ikiwa zaidi ya 300, wavuvi kutakiwa na halmashauri kulipia  shilingi 7000 kila mwezi (parking fees).

Aidha TRA hukusanya kwa wavuvi wa dagaa shilingi 2000 kila debe huku boti zinazonunua au kupakia samaki kwenye eneo hilo kulazimika kulipia  mapato ya shilingi laki mbili hadi tatu kutegemea na na ukubwa wa boti kila inapojaza samaki.   
  
Mwenyekiti wa kijiji cha Lushamba, Deus Magumba alipoulizwa kukosekana kwa huduma ya afya visiwani alidai kuwa hilo hawezi kulizungumzia kwasababu nayeye amelikuta ingawa kipaumbele chao kwasasa ni kujenga shule ya msingi eneo la katika Kitongoji cha Kanyara.

“Hata mimi niliwahi kuuliza nikaambiwa na Halmashauri kwamba wanataka tufanye ili wao wamalizie, sasa ukimwambia mwananchi achangie ujenzi ili serikali ituunge mkono anaona kama anaibiwa ukizingatia kuwa sasa hivi tunataka kuchangia shule mpya,” anasema.

Juhudi za kumtafuta diwani wa Kata ya Bulyaheke, Bageti Ngere Nyuki zimegonga mwamba baada ya kukwepa kukutana na mwandishi mara kadhaa alipopigiwa simu huku akitoa visingizio vingi wakati mwingine akidai yupo mbali au kwenye kelele hawezi kuzungumza.

Naye Mbunge wa Jimbo la  Buchosa, Charles Tzeba , alipoulizwa kuhusiana na kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii katika visiwa hivyo alidai kuwa yeye ni mbunge wa kitaifa anayesimamia bajeti kuu mengine hayo waulizwe viongozi wa Halamashauri.

“Kwani wee mwandishi nani amekutuma ukachunguze hayo? Kwanza ujue kuwa mimi nimechaguliwa kama mbunge kipindi hiki hivyo hali nimeikuta kama ilivyo labda uwasiliane na viongozi wa  Halmashauri wakueleze wana mpango gani na maeneo hayo kwasababu wanabajeti zao,” anasema Tzeba.
 
Mbunge huyo ambaye ni Naibu Waziri wa Uchukuzi alisema kuwa kazi yake nikusimamia bajeti ya kitaifa namna inavyotekelezwa na serikali na masuala ya jimbo wanaopaswa kuyashughulikia ni Diwani pamoja na mwenyekiti wa halmashauri kwa kushirikiana na mkurugenzi.

Hata hivyo juhudi za kuwapata viongozi hao zinaendelea kwani mwandishi amefika mara kadhaa kwenye ofisi za  Halmashauri hiyo na kushindwa kuwaona viongozi hao wala kupata  mawasiliano yao.

Mwwandishi ni Mkurugenzi wa shirika huru la habari Tanpress, anapatikana kwa 0656938315


No comments:

Post a Comment