17 December 2012

TASAF yazidi kuongeza ya matumaini kupunguza umaskini



Na Eliasa Ally, Iringa

MIRADI ya maendeleo mijini na vijijini ni kiunganishi baina ya serikali na wananchi wake kutokana na umuhimu wake katika maisha yao ya kiala siku.


Utekelezaji wake hushindwa kutokana na baadhi ya watendaji kutumia fedha kwa maslahi binafsi badala ya kuwasaidia walengwa.

Usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ni kichocheo cha maendeleo katika jamii kwa ni pia hutoa ajira za muda wakati wa utekelezaji wake.

Maendeleo ambayo kwa sasa katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa yamefanyika na yanaendelea kufanyika yanatokana na Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, yanayowafikia wananchi wenyewe wa maeneo ya vijijini kutokana na TASAF kuwashirikisha wananchi katika kuibua miradi yenyewe ambayo huwasaidia kukuza vipato vyao.

Miradi hiyo inayofanywa na wananchi huleta dhana kwa wananchi wenyewe na hali hiyo sasa wananchi wanaiona serikali ipo kwa ajili yao kutokana na kuwashirikisha utendaji mzima kuanzia ngazi ya kuibua miradi, kufanya vikao vya kuandaa miradi kuipeleka TASAf, kuunda kamati za utendaji ambazo zinatolea ripoti kila mwezi.

Hali hiyo inawapa motisha wananchi wa vijijini na kuona kuwa miradi ya moja kwa moja ambayo serikali kupitia TASAF wanatoa fedha za kuwawezesha kujenga miradi.

Uchunguzi wa Majira katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Iringa Vijijini, katika kata za Kiwere, Idodi na Mtera na kubaini miradi ambayo ina mashiko kwa wananchi ni ile ambayo imefanywa na serikali kupitia TASAF ambapo hoja kubwa naya msingi ni ushirikishwaji wa wananchi moja kwa moja katika kuiibua na shughuli nzima za kufanikisha ukamilishwaji wa miradi hiyo.

Katika kata ya Idodi, imeweza kushirikiana moja kwa moja na wananchi kwa kuibua mradi wa kujengewa mifereji ya kilimo cha umwagiliaji wa mpunga kutokana na eneo la kata hiyo kushambuliwa mara kwa mara na hali ya uhaba wa mvua za kutosha, ambapo vijiji vitatu vya Mahuninga, Makifu na Idodi tayari vimejengewa miradi ya mifereji na sasa wana uhakika wa kilimo cha uhakika.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Idodi, Augustino Mato, Benadetha Mkongwe, Lulambililo Mkuye Veronica Kasuva, Cosmas Mtali na Selina Msambusi wanathibitisha kuwa miradi ambayo inaibuliwa na wananchi wenyewe na kusaidiwa na serikali kupitia Tasaf katika kuijenga, imekuwa na mafanikio lukuki na wananchi sasa wanabaini kuwa kumbe miradi inayofanyika vijijini ni ya wananchi wenyewe.

“Sisi wananchi tumeibua miradi yetu lakini serikali kupitia mfuko wa maendeleo yake ya Tasaf tumeweza kusaidiwa fedha za kukamilisha na kujenga miradi ya kujenga mifereji ya kilimo cha umwagiliaji, sasa tuna uhakika katika vijiji vyetu kulima kilimo cha uhakika, tunatarajia kunufaika kwa kupata mazao mengi na uchumi wetu kukua kwa asilimia 50 na tutaweza kujenga nyumba bora, kusomesha watoto wetu na kujikimu kimaisha”, anasema Abisai Kisakanike mkazi wa kijiji cha Mahuninga.

Katika kijiji cha Mfyome kata ya Kiwere wananchi waliibua mradi wa kujinurusu na uchumi ambapo walianzisha ufugaji wa nyuki ili wavune mazao ya asali ambapo jumla ya mizinga ya nyuki 75 imeweza kuwekwa kwa ajili ya wananchi waliounda vikundi na wameanza kuvuna asali na kujipatia kipato.

Wakizungumzia mradi wa ufugaji wa nyuki baadhi ya wananchi,  Romoso Ndulele, Marko Kilongo na Thomas Mhapa wanasema kuwa mradi huo kwa sasa unawaingizia kipato kikubwa na wameweza kuondokana na hali ya kukabiliwa na umaskini katika vijiji vyao tofauti na kabla walipokuwa hawajaibua mradi huo na Tasaf kuwasaidia fedha za kununulia mizinga.

“Mazao ya nyuki ya asali na nta yana soko kwa kuwa wananchi wengi wanajua asali haiwezi kuongezwa wala kupunguzwa ubora wake, wateja wapo kwa sasa tunauza  debe moja la asali shilingi 6000 hadi 8500 na mzinga mmoja unatoa madebe sita hadi nane ambapo kwa mwaka tunavuna asali mara tatu kwa hiyo kiuchumi endapo unakuwa na mizinga zaidi ya kumi inakuletea faida kubwa”, anasema Diwani wa kata ya Kiwere Pascal Mwamwano.

Wakazi wa kata ya Mtera wakizungumzia miradi ya Tasaf wanasema kuwa serikali kupitia miradi hiyo inawahamasisha moja kwa moja kutambua na kuwafanya sasa wananchi wa vijijini wayathamini maisha yao, waliibua  miradi ya ujenzi wa vizimba vya kukuzanya taka ngumu maeneo ya vijijini ili kuboresha usafi wa mazingira.

Miradi ni pamoja na kushiriki shughuli za maendeleo kwa wananchi wa vijiji vya Mtera na Migori Gilbert Mwenga, Bonifas Kidongosisi, Mohamed Kanu, Zuena Sana na Romanus Sambala wanasema kuwa kufanikisha kwa ujenzi wa vizimba vya kukusanya taka ngumu kumewezesha kusafisha katika vijiji vya Migori na Mtera sasa kuwa na mazingira safi na bora zaidi kwa wananchi wenyewe.

“Kiuhalisia swala la usafi kwa wananchi hususani wakazi wa vijijini ni muhimu, sisi wananchi kwa pamoja tuliibua mradi wa kukabiliana na usafi, baadaye tulipeleka andiko la mradi wilayani katika idara ya Tasaf ambao kwa sasa wametujengea vizimba 10 na dambo moja pamoja na kupatiwa 'power tiller' ya kusomba taka”, anasema, Alam Mbilinyi Mwenyekiti wa kijiji cha Mtera.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini, Pudenciana Kisaka anasema miradi ambayo imeibuliwa na wananchi na kusaidiwa fedha na Tasaf kuwa ni ujenzi wa mifereji mitatu ya kilimo cha umwagiliaji katika kata ya Idodi, kijiji cha Mfyome, kata ya Kiwere, kata ya Mtera katika vijiji vya Mtera na Migori wananchi waliibua na kujengewa mradi wa vizimba vya kukusanyia taka ngumu na baadaye kuzipeleka kwenye dambo kuu.

Anafafanua kuwa katika ujenzi wa mifereji mitatu ya kata ya Idodi imejengwa katika vijiji vitatu ambapo umegharimu milioni 107,537,008 katika kijiji cha Mahuninga mfereji umegharimu milioni 35,762,568, ambapo katika kijiji cha Makifu ujenzi wa mfreji umegharimu milioni 35,982,522 na kuwa katika kijiji cha Idodi ujenzi wa mfereji wa kilimo cha umwagiliaji umegharimu shilingi milioni 35,793,918.


Akizungumzia mradi wa ufugaji wa nyuki,anasema kuwa jumla ya mzinga ya nyuki 75 imechongwa na kukabithiwa kwa wananchi ambao waliunda vikundi vyao na kuibua mradi huo ambapo aliongeza kuwa katika kufanikisha shughuli nzima ya mradhi kuwa jumla ya milioni 9,896,760.

Aliongeza kuwa katika mradi wa ujenzi wa vizimba vya kutunza taka ngumu, katika kata ya Mtera katika vijiji vya Migori na Mtera vizimba vitano vimejengwa katika kijiji cha Migori ambapo vimegharimu milioni 35,946,350 ambapo katika kijiji cha Mtera wananchi wameweza kujengewa vizimba vya kutunzia takataka ngumu vitano vyenye thamani ya milioni 35,809,950 ambapo pia katika eneo la Mtera limejengwa dampo kuu ambalo litatumika kusombelea taka zote na kuzitibu.





No comments:

Post a Comment