17 December 2012
UVCCM waingia wasigana na umoja wa makanisa
Na Patrick Mabula, Kahama,
UMOJA wa Makanisa wa Wilaya ya Kahama umelaani kitendo cha Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM ) kuvamia na kufanya fujo kwenye eneo la Kanisa la Anglikana lililopo eneo la Nyasubi mjini hapa, ambapo walitishia kuvunja majengo ya shule inayojengwa kwa madai kiwanja chama (UVCCM).
Kauli hiyo ilitolewa siku moja baada ya vijana wa UVCCM wa wilaya, wakiwa na viongozi wao kuandamana hadi eneo la Kanisa hilo wakitoa maneno ya vitisho na kuzuia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Katibu wa Umoja wa Makanisa wa Wilaya ya Kahama, Mchungaji Williamu Mgunda, alisema wanalaani tabia hiyo ya kujichukulia sheria mkononi huku vijana hao wakitoa vitisho kwamb wapo tayari kumwaga damu.
Katibu wa Kanisa la Anglikana, Edward Nelson, alisema vijana wa UVCCM walivamia kanisa hilo ambalo linajengwa na kutoa vitisho kwa mafundi.
Alisema wakati wakifanya fujo walikuwa wakitamka maneno kuwa wao ndiyo Serikali na wako tayari kumwaga damu ili kuhakikisha jengo hilo linabomolewa.
Mchungaji Msaidizi wa Kanisa la Anglikana Mchungaji, Shemu Elia, alisema amesikitishwa na kitendo hicho kinachoweza kusababisha uvujifu wa amani.
Mwenyekiti wa vijana wa CCM wa Wilaya ya Kahama, Solomon Mataba, alikiri kutokea tukio hilo na kwamba huo ni mkakati wa kufuatilia mali za chama. Alidai kuwa jengo hilo limejengwa katika kiwanja chao
kinachopakana na kanisa hilo.
Katibu Mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Kahama,Masod Melimeli, alisema hawako tayari kuona mtu akichukua mali za chama na kwamba atakaye fanya hivyo watamshughulikia kikamilifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment