NI wazi kuwa hivi sasa hali ya maisha imekuwa ngumu kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na kusababisha baadhi ya watu kuishi maisha ya kubahatisha.
Hali hii pia imekuwa ikichangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa ikiwemo vyakula na kusababisha watu kuishi maisha ya kubahatisha.
Nionavyo hali ya kupanda kwa bei za bidhaa na vyakula inasababishwa na utandawazi ambapo pia kimsingi unaweza kuelezwa kuwa ni mchakato wa kuunganisha uchumi, siasa, jamii, uhusiano wa tamaduni baina ya nchi.
Utandawazi unaifanya dunia kuwa kama kijiji kimoja kisicho kuwa na mpaka ambapo pia unasisitiza uondoaji wa vikwazo vya kibiashara na kuifanya dunia kuwa soko moja.
Ni wazi kuwa utandawazi unahimiza soko huria, demokrasia, utawala bora, usawa wa kijinsia, haki za binadamu, utunzaji wa mazingira miongoni mwa jamii husika.
Pamoja na kuwepo hali hiyo kuna matatizo mengi ambayo yamesababishwa na kuwepo kwa soko huria na kufanya maisha ya wananchi kuwa ya kubabaisha kutokana na hali hiyo.
Soko huria limechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa bei ya vyakula hivyo hali hiyo imeongeza shida kwa wananchi hasa wa kipato cha chini na kuwaweka katika uwezekano mkubwa wa kupata utapiamlo kutokana na kushindwa kumudu milo mitatu.
Hali ya kushindwa kumudu pia imechangia baadhi ya wananchi kulazimika kula vyakula vya aina moja kila kukicha kutokana na umasikini walio nao hali ambayo kiafya ni hatari.
Hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wakihojiwa kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa ambapo walisema hali hii inatokana na uhuru wa biasahara unaosababishwa na kuwepo kwa soko huria.
Baadhi yao walisema kuwa, wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakinunua vyakula vingi kwa bei ya chini na kusubiri vyakula hivyo vipitwe msimu na kuvitoa na kuviuza kwa bei ya kulangua.
Nionavyo, kutokana na hali hii bado mkulima anakuwa hajakomboka katika umaskini kwani hulazimika kuuza mazao yake kwa bei nafuu kwa wafanyabiashara wakubwa huku yeye akiwa ametumia nguvu nyingi kwa kilimo na kunufaika kidogo.
Kufanya hivyo ni sawa na wafanyabiashara wakubwa kuitumia nafasi yao kumkamua mkulima kwa kununua bidhaa zao kwa bei nafuu na kuzificha kwa ajili ya kungoja ziadimike na kuzilangua.
Ni wazi kuwa awali bei ya maharage ilikuwa ikiuzwa kwa sh 1600 kwa kilo lakini sasa hivi hali ni mbaya kwani kilo hiyo ya maharage huuzwa kwa sh.2000.
Unga wa sembe ulikuwa ukiuzwa kwa sh. 1,000 na sasa bei ya unga kwa kilo ni sh 1300 hadi 1,500 wakati mchele uliokuwa ukiuzwa kwa sh.2,200 hadi 2,500.
Kwa upande wa mafuta ya kula yalikuwa yakiuzwa kwa sh 13,500 kwa lita tano hadi sh. 15,000 na kufanya hali ya watu hasa wa kipato cha chini kuwa hoi bin taabani.
Nionavyo hali hii inatokana na kupungua kwa mazao kama mahindi lakini bado si sababu ya kumkandamiza mtu wa hali ya chini wakati wengine wakineemeka kupitia migongo ya watu na kuwaacha wengine kuwa hoi.
Kutokana na hayo ipo haja kwa serikali kusimamia bei za wakulima kwa vitendo ili kunusuru maisha yao na kuwezesha watu wa kipato cha chini kuneemeka.
Pia ieleweke kuwa utandawazi siyo dhana mpya kama inavyotaka kuaminishwa na baadhi ya wasomi mbali mbali hapa duniani, kwani historia inatuambia kuwa utandawazi ulianza enzi za Christopher Columbus alipokwenda Amerika na kuingiza mazao ya miwa, machungwa na uchimbaji mkubwa wa madini.
Afrika iliingizwa katika utandawazi rasmi enzi za biashara ya utumwa iliyojulikana kama, 'The Trans Atlantic Slave Trade' Afrika ilifanywa kuwa chanzo cha nguvu kazi ya bei rahisi, ambapo watumwa walipelekwa bara la Amerika katika mashamba na migodi mikubwa, baada ya mapinduzi ya viwanda biashara ya utumwa ilionekana kutokuwa tena na faida na hivyo ilisitishwa.
Waafrika walionekana kuwa wanaweza kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya Ulaya na pia kuwa soko kwa bidhaa za viwandani kwa hiyo mnamo mwaka 1884 ulifanyika makutano Ujerumani, maaarufu kwa jina Mkutano wa Berlin.
Mkutano huu ulikuwa mahususi kuligawa bara la Afrika kwa watawala mbali mbali, makoloni yalihimizwa kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya Ulaya, kwa mfano makoloni yaliyokuwa chini ya Muingereza yalizarisha kwa ajili ya nchi hiyo.
Ni wakati wa kuweka mkakati dhabiti kuhimili hali ngumu ya maisha kwa kuwapatia wananchi ujuzi ili kujikomboa kwa kubuni miradi ya maendeleo.
Hali hii ikiendelea vitendo vya ukabaji na kujichukulia sheria mkononi kwa wananchi hali inayohatarisha amani ya nchi.
No comments:
Post a Comment