27 December 2012

Maaskofu waonya ukimya wa serikali *Wataka iwachukulie hatua wanovuruga amani *Malasusa akemea matumizi ya silaha za moto



Na Waandishi Wetu

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa, amewataka watawala nchini
kuacha kutumia silaha za moto ili kulinda amani iliyopo.


Alisema amani inatengenezwa kwa njia za uvumilivu badala ya
kutumia silaha za moto ambapo jamii inapaswa kutambua kuwa,
amani haitafutwi kwa vurugu au maandamano yasiyo na tija.

Dkt. Malasusa aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Azania Front na kusisitiza kuwa, upo umuhimu wa kila mtu bila kujali
dini yake kudumisha amani na mshikamano uliopo.

Alisema Sikukuu ya Krismasi ambayo huadhimiswa na Wakristo wote duniani, ina ujumbe wa Mungu kupitia malaika wake hasa katika suala zima la amani na mshikamano.

“Ni imani yangu kuwa, sikukuu hii itaadhimishwa kwa amani na upendo kwa Wakristo wote, mwaka 2013 utakuwa wa amani kwa watu wote kutoka kwa Mungu na kuheshimiana,” alisema.

Kwa upande wake, Paroko la Kanisa la Mtakatifu Peter, Joseph Mosho, lililopo Osterbay Dar es Salaam, aliwataka Watanzania kumcha Mungu kila wakati ili kuiepusha nchi na changamoto mbalimbali zinazotaka kulikabili Taifa.

Alisema vipo vishawishi vingi ambavyo Wakristo kama wasipokuwa makini, wanaweza kuliingiza Taifa katika machafuko, umaskini na kukwamisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Paroko Mosha aliyasema hayo katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi kanisani hapo na kusisitiza kuwa, Tanzania ni nchi ya amani kwa sababu watu wake wanapenda kumuomba Mungu kila wakati.

“Ni vyema tukawa wapole na watulivu, zipo baadhi ya nchi ambazo zipo katika machafuko na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia, Sikukuu ya Krismasi ni ya amani, inayotoa fursa kwa familia kukaa pamoja na kujadili mambo yanayompendeza Mungu,” alisema.

Naye Padre Wilfrid Dino wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam, alisema ukatili dhidi ya watoto umeongezeka hivyo kama jamii isipopiga vita vitendo hivyo, itabeba mzigo huo.

Padre Dino aliyasema hayo katika ibada ya Sikukuu ya Krisimasi iliyofanyika Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa, maandiko matakatifu yanatufundisha jinsi ya kuwalea watoto vizuri na kuwatunza lakini hivi sasa binadamu wamekuwa wakatili
na kukiuka maagizo waliyopewa na Mungu.

“Matumboa ya akina mama, hivi sasa yamekuwa makaburi ya watoto, madaktari kwa ukatili mkubwa wamekuwa wakishiriki kuwaua watoto kwa kuwakata na mikasi (kutoa mimba).

“Kama mama Maria angefanya hivyo, leo hii tusingeadhimisha sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo,” alisema.

Alisema kwa hali ilivyo sasa, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vimeshika kasi na si janga la kitaifa pekee bali ni la dunia nzima hivyo ni vyema wanawake, wanaume na madaktari watubu kwa kuandika barua na kuorodhosha watoto waliofanyiwa ukatili huo.

Aliongeza kuwa, ni kawaida ya mtu mzima kujiokoa anapopatwa na tatizo linalohatarisha maisha yake hivyo mtoto naye huangaika pale anaposhambuliwa kwa mikasi tumboni kama wahusika wangeona jinsi anavyohangaika, wangeacha kufanya hivyo.

“Mtoto anapouona mkasi, hujitahidi kujibanza pembeni ya tumbo la mama usimfikie na kupiga kelele kuomba msaada ili asiuawe lakini kwa kuwa sauti yake haisikiki, hujikuta akinyimwa fursa ya kuja duniani kuungana na watoto wenzake,” alisema.

Padre Dino alisema, wapo baadhi ya wasichana wanaolalamika kuwa wakienda shule, hawaoni vizuri lakini wakitoka eneo hilo wanaona na baada ya kuwadadisi, mmoja wapo alimwambia alitoa mimba nne na mwingine nane ndio maana walikuwa wakiteseka.

“Mambo haya ambayo yanafanywa na binadamu ndio chanzo cha majanga yanayotokea nchini pamoja na kuteseka kwa wanawake,” alisema Padre Dino.

Askofu Martin Shao

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Martin Shao, ameiomba Serikali
itoe tamko lake dhidi ya vitendo vya udhalilishwaji, kashfa na
kejeli dhidi ya Wakiristo vinavyofanywa na baadhi ya vikundi
vya Kiislamu na kutishia kuvuruga amani ya nchi.

Askofu Shao aliyasema hayo kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro na kuongeza kuwa, upo ushahidi wa mikanda ya video na DVD ambayo inahusu kukashifiwa kwa Wakiristo.

“Wapo baadhi ya watu wanaodai kuwa, nchi inaongozwa kwa Mfumo wa Kikristo jambo ambalo halina ukweli wowote na linapaswa kukemewa ili lisiweze kuvunja mshikamano uliopo.

“Kauli hizi ni mbaya kwa mustakabali wa kitaifa hivyo ni jukumu la Serikali kukemea ili kuilinda misingi imara iliyoachwa na waasisi wa Taifa hili,” alisema Askofu Shao.

Aliongeza kuwa, tayari Jumuiya ya Kiksristo nchini imetoa kauli dhidi ya vitendo hivyo na kutaka majibu ya Serikali kwani wakati mwingine kukaa kimya ni ishara ya kuunga mkono kauli ambazo hazina nia njema na umoja wa kitaifa.

“Tusibweteka na amani tuliyonayo ambayo inaweza kutoweka wakati wowote kama hatutafuata misingi iliyoachwa na waasisi
wetu, yale yaliyotokea katika nchi za Kenya na Congo (DRC), yanaweza kutokea kwetu pia,” alisema Askofu Shao.

Alisema Watanzania wanaopenda amani ni wengi na wapo katika madhehebu ya dini, wanasiasa na wataalamu wa fani mbalimbali, lakini ni vyema jamii ikaepuka roho ya udini na ufisadi.

Moshi Kilimanjaro

Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mhashamu Isack Amani, ameelezea kusikitishwa kwake na
ukimya wa Serikali katika kufuatilia dalili, matamshi na
vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu
wanaodaiwa kuwa na imani kali za kidini.

Alisema wapo baadhi ya watu wanaotoa matamshi ya hatari kwa kivuli cha dini katika vyombo vya habari na kudai Maaskofu wote lazima waangamizwe lakini Serikali imekaa kimya bila kutoa tamko.

Askofu Amani aliyasema hayo juzi katika ibada ya mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika kwenye Kanisa la Kristu
Mfalme, lililoko Moshi Mjini, mkoani humo.

Alisema matamshi kama hayo ukichanganya na matukio ya hivi karibuni ya uchomaji wa makanisa, kuharibu mali kitika madhehebu na ukimya wa Serikali, inaleta mashaka kwa wale wanaoathirika na kuamsha hisia mbaya za kutaka kulipiza kisasi.

“Binafsi nasikitishwa na matamshi yenye kukejeli kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na makanisa katika kuboresha elimu na sekta ya afya nchini kabla na baada ya uhuru.

“Pia nasikitishwa na watu wanaotoa maneno ya kashfa dhidi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye amefanya kaiz nzuri
wakati wa uhai wake kwa kuyatoa maisha yake ili kutetea umoja
wa nchi yetu hivyo kumkashifu kwa njia yoyote ni kuipotosha
jamii ya sasa jambo ambalo ni dhambi kubwa,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kupuuza maneno yanayoenezwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa mfumo Kristu ambayo hayana ukweli wowote, haijawafi na haitaongozwa kwa mfumo huo na wale wanaotoa madai hayo wana lengo la kuwagawa Watanzania.

Alisema Tanzania Bara baada ya kupata uhuru wake, iliaminiwa duniani kote kuwa ni nchi ya amani na nchi nyingi zenye ambazo zilikuwa na machafuko, raia wake walikimbilia nchini.

“Hivi sasa tupo njia panda, ishara ya kutoweka kwa amani yetu inaanza kuonekana, hili linakatisha tamaa, wapo baadhi ya watu wanaotaka kutumia vurugu hizo ili kutimiza malengo na tamaa
zao mbaya,” alisema Askofu Amani.

Aliongeza kuwa, “Hali inayoendelea sasa si ya kufikirika ambapo Tanzania haina kinga ya kuepusha machafuko zaidi ya Serikali yetu kutoa tamko ambalo litasaidia kudumisha amani iliyopo,” alisema.

Aliiomba Serikali na Watanzania kwa ujumla, kuhakikisha tabia na mienendo ya kuchukiana na kukashifiana, inakomeshwa badala yake kila mmoja amuheshimu mwenzake.

Aliwataka viongozi wa dini kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa ili kudhibiti vikundi vyenye muelekeo wa kuleta vurugu nchini pamoja na kulinda amani iliyopo.

Ibada Zanzibar

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Michael Henry Hafidh, amesema wakati umefika kwa viongozi wa kisiasa
na dini wanaoeneza chochoko za ubaguzi wa kidini, kudhibitiwa kwa maslahi ya Taifa.

Alisema viongozi wa kisiasa na dini wanawajibu wa kulinda amani na umoja wa kitaifa lakini hivi karibuni, wameanza kusahau wajibu wao, kusababisha uvunjifu wa amani na uharibifu mkubwa wa mali za umma na watu binafsi.

Askofu Hafidh aliyasema hayo Zanzibar jana katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi na kuongeza kuwa, vipo vikundi vya uhalifu vinavyotumia kivuli cha dini ya Uislamu kuhatarisha amani hivyo umefika wakati wa Serikali kudhibiti vitendo hivyo.

Alisema Tanzania ni nchi ya amani hivyo jamii lazima ijifunze kutoka katika nchi nyingine kama Kenya, Naigeria ambazo ziliwai kukabiliwa na machafuko kutokana na tofauti za kidini, kisiasa na ukabila.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, Umoja wa Makanisa umeamuwa kutoa tamko kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Askofu Hafidh alisema, upo umuhimu wa waumini wa dini ya Kikristo kuilinda na kudumisha amani iliyopo kwa kujiepusha na mambo ambayo yapo kinyume na maadili ya Mtanzania.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Zanzibar, Dickson Kaganga, aliwataka waumini kuwa na moyo wa subira na kusahau mambo yaliyopita kama uchomaji moto makanisa na kuwasamehe waliofanya vitendo hivyo.

“Mungu alitupenda sisi na kutuletea Yesu ambaye alisamehe
yote aliyotendewa, kwanini wanadamu tushindwe kusamehe yaliyotokea, tumefanyiwa mambo mengi mwaka huu ndio
maana nakumbushia sual la msamaha,” alisema.

Naye Muinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Zanzibar, Jimbo la Mission, Usharika wa Mwanakwerekwe, Cloud Marck Mhina, alisema sikukuu hiyo
ni muhimu kwa kila Mtanzania kutenda mema na kuwataka
waumini wa kanisa hilo kuacha vitendo viovu.

Askofu Dkt. Alex Mkumbo

Askofu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, Dkt. Alex Mkumbo, amewataka Watanzania kudumisha amani ambayo ndio msingi wa mafanikio, ustawi wa maisha yao.

Dkt. Mkumbo aliyasema hayo mkoani Singida jana katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Ushirika wa Makao Makuu ya kanisa hilo mjini humo.

Alisema wote waliokabidhiwa dhamana ya kutoa huduma mbalimbali katika ofisi za umma, wanapaswa kufanya kazi
zao bila upendeleo ili kuondoa manung’uniko.

Aliongeza kuwa, ni muhimu kwa kila mtu kujishusha kama
mwokozi wao alivyozaliwa katika mazingira duni ili Mungu
apate kumwinua na kumpa baraka katika maisha yake.

“Amani huletwa kwa njia ya upendo na kujaliana jambo ambalo
linaifanya jamii kuwa na utulivu na kufanya kazi zinazoleta tija,” alisema Askofu Mkumbo.

Padre Mietek

Padre Mietek wa Kanisa la Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea, Dar es Salaam, kutoka nchini Holand, amewataka
waumini wa kanisa hilo kuwa mfano wa kuigwa kwa kueneza
habari za Mungu na kuzaliwa Yesu Kristo.

Alisema hali hiyo itasaidia kueneza kizazi kinachojua habari
za Mungu kwa siku za usoni na kuongeza kuwa, si jambo la kushangaza kusikia kuna watu ambao hawamjui Mungu.

“Ndugu zangu mliohudhuria ibada hii, nawaomba mkafanye haya ninayowaagiza ili jamii kubwa iweze kujua mema mengi ambayo yamefanywa na Mungu.

“Wanadamu tunajisahau lakini Yesu anatukumbuka na kututafuta kila mwaka ifikapo siku kama hii na kuadhimisha kuzaliwa kwake akitukumbusha kuwa yupo na anatupenda,” alisema.

Imeandikwa na Heckton Chuwa, Grace Ndossa, Rehema Maigala, Goodluck Hongo, Mwajuma Juma, Martha Fataely, Damiano Mkumbo na Anneth Kagenda.

1 comment: