27 December 2012
Mafundisho ya ibada ya Krisimasi yawe fundisho
JUZI na jana wakristo duniani kote waliungana kusherekea Sikukuu ya Krisimasi, ambayo si siku ya kiistoria kwao.
Kwa waliohudhuria ibada ya sikukuu hiyo au kufuatilia mahubiri kwenye vyombo vya habari watakubaliana na sisi kuwa kikubwa kilichohubiriwa na viongozi wa dini ni kuhimiza upendo, kuvumiliana ili kudumisha amani iliyopo nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa, alienda mbali zaidi akisema amani itengenezwe kwa njia ya kuvumiliana na si watawala kutumia risasi kutengeneza amani.
Kwa ujumla mahubiri ya Krisimasi yamekuwa na mafundisho mengi ambayo Watanzania wanatakiwa kuyazingatia ili kudumisha amani ambayo nchi yetu inajivunia kwa miaka mingi kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine.
Tunawaunga mkono viongozi wetu wa dini kwa kuhimiza misingi ya kuvumiliana kwa ndiyo njia pekee ya kutufanya tuishi kwa kupendana na kuonana ndugu bila kuulizana kabila, dini wala rangi. Kuvumiliana ndiko kumesaidia kuepusha Tanzania isitumbukie kwenye machafuko pale panapotokea viashiria vya kuvunjika kwa amani.
Mfano mzuri wa kuvumilia kunavyoweza kudumisha amani ni tukio la hivi karibuni lililotokea Mbagala wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo mtoto wa kikristo alidaiwa kudhalilisha kitabu kitakatifu cha Kuran.
Tukio hilo lilisababisha vurugu ambapo watu wanaodaiwa kuwa waumini wa dini ya kiislamu walichoma moto makanisa na kuharibu mali.
Hali hiyo ilikuwa ni hatari endapo upande mmoja usingeonesha uvumilivu. Tukio hilo linatupa picha kamili ya kwa nini viongozi wetu wa dini wanahimiza kuvumiliana ili nchi yetu izidi kuwa na amani.
Tuna kila sababu ya kulinda amani yetu kama tunavyolinda mboni za macho yetu. Amani tunayoichezea leo ikivunjike itakuwa si rahisi kuirejesha. Tunasema hivyo kwa sababu tunatambua kwamba ni rahisi kuvunja amani ndani ya siku moja lakini kuirejesha inachukua muda mrefu na hata pale inapopatikana inaacha mbegu ya chuki, kutokuaminiana na wakati mwingine kulipizana visasi.
Kamwe Watanzania tusikubali kutumika na kupelekwa katika mazingira ya kuishi kwa mashaka. Wale wanaoona amani si jambo la msingi kwao waelimishwe ili waweze kujua kwamba wanachokichezea ndiyo tunda la roho.
Inawezekana Watanzania tukaendelea kuishi kwa mshikamani miaka mingine 51 ya uhuru wetu. Njia pekee ya kutufikisha huku ni kuzingatia yale tunayofundishwa na viongozi wa dini ikiwa ni pamoja na kutii sheria za nchi bila shuruti. Bila amani hakuna jambo lolote linaweza kutendeka ndani ya jamii ndiyo maana tunahimiza Watanzania wote kuhakikisha mafundishi ya ibada ya Krisimasi yanakuwa fundisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
NYUMBA ZA IBADA ZIMEACHA KUZUNGUMZIA MASUALA YA DINI KINACHOFANYIKA NI SIASA ,KUJADILI KATIBA WAKATI MWINGINE TUNAFIKIRIA JE WAMEAMUA KUSHIRIKI SIASA SINA UHAKIKA HUKO MBINGUNI TAWALA ZA DUNIA ZINA NAFASI MATOKEO YA SIASA KWENYE NYUMBA ZA IBADA NA BOKO HARAM HUKO NIGERIA ,AL SHAABAB HUKO SOMALIA SINA UHAKIKA ILE KANDA YA VIDEO INAYOONYESHA UNYAMA UNAOTENDEKA HUKO SOMALIA VIONGOZI WA DINI WANAIONAJE IWAPO BINADAMU ANACHINJWA KAMA KUKU HUKU DUA ZINASOMWA KAMA KWENYE MAKANISA YOTE HAKUNA ALIYELAANI BASI KUNA HATARI HATA TANZANIA TUTAFIKIA YALE YANAYOTENDEKA MALI KASKAZINI MBONA MAPADRI WANAUAWA TUNATOA MAJIBU RAHISI TU NI MAJAMBAZI KULE IRINGA HIVI HIVI NI MAJAMBAZI DALILI ZA MVUA NI MAWINGU
ReplyDelete