17 December 2012

Utekelezaji ahadi, usimamiaji wa maamuzi ukurejesha imani kwa wananchi


Na Suleiman Abeid

MOJA ya mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na kupigiwa kelele na watanzania wengi ni suala la kutotekelezwa kwa ahadi walizoahidiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.


Mbali ya kutotekelezwa kwa ahadi hizo pia lipo suala la Chama hicho kushindwa kusimamia maamuzi yake mbalimbali inayoyafikia hali ambayo imesababisha baadhi ya wanachama wake kuilalamikia.

Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa baadhi ya wananchi kupoteza imani juu ya chama hicho ambacho kimekaa madarakani kwa zaidi ya nusu karne tangu enzi za TANU na kujikuta wakiviunga mkono vyama vya upinzani wakitegemea kuwa mkombozi wao.

Ni wazi kwamba suala la utekelezaji wa ahadi yoyote inayotolewa kwa mtu ni suala muhimu ambapo mtoa ahadi hupaswa kuwa makini pale anapokuwa amewaahidi watu kuhakikisha anatekeleza ahadi aliyoitoa vinginevyo watu hao wataacha kumwamini.

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa mwaka 2010 vyama mbalimbali vya siasa vilitembea kila kona ya Tanzania kunadi sera pamoja na ilani zao za uchaguzi sambamba na kuwaahidi watanzania kwamba iwapo watawapa ridhaa ya kuongoza dola wataweza kuwatekelezea ahadi hizo.

Kila mgombea wa chama cha siasa kilichoshiriki katika uchaguzi huo alijitahidi kumwaga sera na kuelezea kwa ufanisi mkubwa kwa nini anaomba chama chake kichaguliwe na kuonesha jinsi gani watakavyotekeleza ilani ya uchaguzi waliyoinadi kwa wananchi.

Chama Cha Mapinduzi ndicho kilichoonekana kuwa na sera nzuri sambamba na ilani yake ya uchaguzi ambayo ilinadiwa na wagombea wake akiwemo mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete aliyewathibitishia watanzania kwamba kati ya ilani zinazodaiwa na vyama vya siasa, inayotekelezeka ni ile ya CCM.

Katika kipindi hicho Rais Kikwete alisema iwapo chama chake kitapewa ridhaa na watanzania ya kuendelea kukamata dola kitahakikisha kinakuwa ni chama sikivu kwa shida mbalimbali za watanzania kwa kuhakikisha kinawaletea maendeleo na maisha bora.

Kwa kawaida ilani ya uchaguzi hupaswa kutafsiri na kuelezea sera za chama husika kuhusu maeneo muhimu ya siasa, uchumi na jamii.

Ilani hupaswa kueleza kwa ufasaha kuhusu mikakati yake ya utekelezaji wa sera zinazonadiwa pindi wagombea wa chama husika watakapofanikiwa kushinda uchaguzi na hutoa ahadi kwa wananchi kuhusu mambo ambayo chama kitayatekeleza.

Kwa kifupi, ni maelezo ya sera katika kipindi husika kwa kuwaeleza wapiga kura ni mambo gani chama kitayatekeleza iwapo kitashinda uchaguzi na kuweza kuunda serikali.

Kwa hali hiyo baada ya CCM kufanikiwa kukamata dola na kuunda serikali, kuna kila sababu ya chama hicho kurejea ahadi zake mbalimbali ilizozitoa kwa wananchi mwaka 2010 kwa kuhakikisha sasa zinatekelezwa kama ilivyoahidiwa.

Hata hivyo hali halisi inaonesha kadri siku zinavyozidi kuyoyoma kuelekea mwaka 2015 wakati wa kipindi kingine cha uchaguzi mkuu nchini na fursa nyingine kwa vyama vya siasa kupita kwa watanzania kunadi sera zao, ahadi nyingi zilizotolewa na CCM mwaka 2010 zitakuwa hazijatekelezwa.

Hii ni kwa kuzingatia ahadi zilizotolewa katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu huo wa mwaka 2010 ambapo kwa haraka ahadi kubwa zilizotolewa na mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais Kikwete ni zaidi ya 70.

Baadhi ya ahadi ambazo Rais Kikwete anapaswa kuzikumbuka ni pamoja na suala la ununuzi wa meli kubwa kuzidi MV Bukoba iliyopata ajali na kuzama mwaka 1996 katika ziwa Victoria, kujenga njia ya reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi mikoa ya kanda ya Ziwa na mkoa wa Tabora kupata maji kutoka ziwa Victoria.

Nyingine ni ujenzi wa uwanja wa ndege huko Misenyi mkoani Kagera, mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme, serikali kujenga upya bandari ya Mbambabay mkoani Ruvuma na ununuzi wa meli mpya katika ziwa Nyasa yenye uwezo wa kubeba tani 400.

Hizi ni baadhi tu ya ahadi zilizotolewa kwa wananchi na mgombea huyo wa CCM ambazo ni wazi kabisa zilichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa wagombea wa CCM katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo chama hicho kupewa ridhaa ya kuunda serikali.

Wakati tukielekea ukingoni mwa utekelezaji wa ahadi hizo kuna kila sababu ya CCM sasa kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wake kwa kuhakikisha pato la taifa hivi sasa linaelekezwa zaidi katika miradi ya wananchi badala ya kulitumia katika utawala kwa kuongeza viwango vya posho za waheshimiwa zinazoongezwa kimya kimya.

Lakini pia nirejee upande wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kunukuu baadhi ya maeneo muhimu yaliyomo ndani yake, ibara au kifungu cha 30 kinachosema, nanukuu;

“Nchi yetu inahitaji uchumi imara na unaokua kwa kasi kubwa na endelevu ili kutatua tatizo letu la umaskini na utegemezi. Ni mapinduzi ya kilimo na viwanda ndiyo yatakayotuhakikishia kufika katika lengo hilo na nchi yetu kuwa na uchumi wa kati,”

Hii ni moja ya ahadi iliyotolewa na CCM kwa watanzania mwaka 2010, sasa ni muhimu kwa chama hicho kukaa chini na kujiuliza je, ahadi hiyo imetekelezwa? Ni kweli mapinduzi ya kilimo kwa wakulima wetu wadogo yamefanyika? Na hali ya viwanda vyetu ikoje mpaka hivi sasa vimeongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo nyuma?

Tukubali kwamba watanzania wa leo siyo wale wa miaka ya 60 na 70, sehemu kubwa ni vijana wapya, vijana wa ‘doticom’ hawa hawadanganywi kwa ahadi hewa zisizo na vitendo, hivyo si ajabu wakaachana na CCM na kujaribu kukiweka madarakani chama kingine mbadala lengo na wao wawe na maisha bora.

Kwa hali hii CCM kama chama tawala na chama kikongwe nchini kinapaswa kubadilika kwa kuhakikisha kinarejea kuwa chama kinachowajali wananchi wake badala ya kukalia malumbano ya wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kuwania nafasi ya urais mwaka 2015.

Rais akiwa ndiye mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba baada ya kutangazwa Rais wa awamu ya tano basi atakayemkabidhi mikoba awe ni Rais anayetokana na chama chake, na hili litawezekana tu kwa CCM kutekeleza kikamilifu ahadi zake kwa watanzania.

Lakini pia lipo suala lingine ambalo linaendelea kukibungua chini kwa chini chama hicho, nalo ni tatizo la kushindwa kusimamia vyema maamuzi yake mbalimbali inayoyafikia.  Yapo baadhi ya maamuzi muhimu yanayofikiwa na chama hicho, lakini cha kusikitisha hayasimamiwi kikamilifu.

Moja ya maamuzi hayo ni suala la kutenganisha uongozi na biashara. CCM tangu enzi za TANU kilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi, enzi hizo mwanachama ye yote bila kujali uwezo wake wa kifedha aliweza kupata fursa ya kuchaguliwa na kuwa kiongozi ambapo wafanyabiashara wakubwa hawakuwa na nafasi.

Enzi hizo ilikuwa ni mwiko kwa kiongozi kuwa na nyumba ya kupangisha au kuwa na hisa katika kampuni kubwa, lakini leo hii viongozi wetu wakuu wakiwemo wabunge na mawaziri ndiyo wafanyabiashara wakubwa katika nchi yetu.

Naamini miiko hii haina nafasi tena ndani ya CCM, mwana CCM ye yote asiye na uwezo wa kifedha hawezi kupata fursa ya kugombea uongozi wowote hasa ule wa ngazi ya juu ndani ya chama chake haki ambayo ni ya kikatiba lakini inavunjwa kwa nguvu ya fedha.

Fungua katiba ya CCM ibara ya 14 kifungu kidogo cha (3) kinasema, nanukuu; pamoja na mambo mengine mwana CCM atakuwa na; “….Haki ya kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi wa CCM na ya kuchagua viongozi wake wa CCM kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za CCM,” mwisho wa kunukuu.

Ukweli kadri siku zinavyokwenda haki hiyo ya msingi kwa kila mwanachama hivi sasa imepotea kabisa japokuwa imebaki kutambuliwa ndani ya katiba lakini utekelezaji wake ni kinyume kabisa kwani tumejionea katika maeneo mengi wana CCM wasio na uwezo wa kifedha wamebaki kuwa watazamaji pamoja na uwezo walionao wa kuongoza.

Ushahidi juu ya hili upo wazi kufuatia mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho uliomalizika hivi karibuni ambapo watanzania tumejionea umwagaji wa fedha uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wagombea ambapo hali hiyo ililalamikiwa na hata aliyewahi kuwa waziri mkuu katika nchi yetu, Bw. Fredrick Sumaye.

Kama hata mtu aliyepata kuwa kiongozi wa ngazi ya juu hapa nchini amelalamikia hali hiyo, je mwana CCM wa kawaida asiye na uwezo wa kifedha ataweza kumudu kugombea uongozi ndani ya chama chake? Ni wazi kwamba suala la kutenganisha uongozi na suala la biashara lilikuwa la muhimu sana.

Ahadi hii kwa ujumla ilikuwa ikigusa pia upande wa viongozi wa kiserikali, lakini jambo la kusikitisha mpaka hivi leo haijaweza kufanyiwa kazi na watu wenye uwezo wa kifedha na wafanyabiashara wakubwa hapa nchini wameendelea kupeta katika nafasi mbalimbali za kiuongozi.

Ni changamoto nyingine kwa chama tawala kulifanyia kazi tatizo hilo, maana siku maskini wataamka kutoka katika usingizi mzito ni wazi watakiadhibu chama hicho kwa kukinyima kura kwa nguvu zote hata kama patakuwepo na mbinu zozote za uchakachuaji wa kura.

Napenda kumkumbusha Rais Kikwete moja ya hotuba zake alizozitoa mwaka 2008 akizungumzia suala la uongozi na biashara, Desemba 31, katika hotuba aliyoitoa kwa wananchi alieleza wazi dhamira ya kubadili mfumo wa sasa wa viongozi wa kisiasa, mawaziri na wabunge kuwa pia wafanyabiashara.

Akihitimisha hotuba hiyo, Rais Kikwete alisema, nanukuu;  “….Hususani napenda kulizungumzia suala la viongozi wa siasa Mawaziri na Wabunge kuwa pia watu wanaojihusisha na shughuli za biashara moja kwa moja. Upo ushahidi wa kuwepo migongano ya maslahi kwa baadhi.”

“Lakini, pia hata pale ambapo hakuna dalili za wazi, hisia za kupata manufaa yanayotokana na nafasi zao hutawala. Matokeo ya yote hayo ni watu kupoteza imani na kutilia shaka uadilifu wa viongozi wetu.”

“Ni jambo lenye maslahi kwa nchi yetu na litasaidia kujenga heshima ya viongozi wa umma mbele ya macho ya wananchi.  Nafurahi kwamba suala hili tumelizungumza katika kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM tulichofanya Dodoma juzi tarehe 29 Januari, 2008 na tumeelewana.  Ni matumaini yangu kuwa sote tutaunga mkono,” mwisho wa kunukuu.

Kwa hali hiyo tunapaswa kujiuliza mkakati huu umefikia wapi, maana leo hii ni takriban miaka minne imepita tangu Rais alipowaahidi watanzania kulifanyia kazi na amethibitisha wazi kwamba limezungumzwa ndani ya vikao vikuu vyenye maamuzi ndani ya chama hicho lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.

Ushahidi mwingine wa CCM kushindwa kusimamia maamuzi yake ni suala la kuwazuia viongozi ambao tayari wana nyadhifa nyingine ndani ya chama kutogombea nafasi za uenyekiti wa wilaya na mikoa na ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya Taifa (NEC) lakini pia nalo limeshindikana.

Sote tumejionea jinsi wana CCM ambao tayari ni mawaziri, wabunge walivyoweza kupeta katika nafasi mbalimbali za ujumbe wa NEC ikiwemo uenyekiti wa CCM wa mikoa na hata pale baadhi ya kamati za siasa zilipoyeungua baadhi ya majina ya vigogo yalirejeshwa kwa milango ya nyuma. (Rejea tukio la wilayani Hanang).

Je! CCM mnapotoa maamuzi yenu huwa mpo usingizini na mnapoamka huyasahau yote?  Maana lengo kuu la kurejesha nafasi za ujumbe wa NEC katika ngazi ya wilaya lililenga zaidi kusogeza huduma karibu kwa wanachama na kwamba mjumbe wa NEC atatakiwa kukaa zaidi katika eneo lake la kazi.  Tutafakari!!!

No comments:

Post a Comment