17 December 2012

Siasa za Mwenyekiti CCM Mkoa na hatima ya wananchi Geita



Na Faida Muyomba

USAFI ni suala muhimu linalostahili kupewa kipaumbele na kila mtu anayechukia uchafu katika mazingira anayoishi kwa kuwa ndio muhimili mkubwa wa maisha ya binadamu.

Ni muhimili muhimu wa maisha ya binadamu kwa maana kuwa, bila usafi hakuna uhai kutokana na ukweli kwamba kila kwenye mazingira  safi daima ni nadra  magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu yanayosababishwa na uchafu kuwepo.

Kutokana na hali hii, ndio maana viongozi wetu mbalimbali, wenye mapenzi mema na wananchi wao wanaowaongoza ikiwemo wizara ya Afya na ustawi wa jamii, wamekuwa mstari wa mbele kuhimiza usafi.

Kila mtu anajua kuwa usafi ndio uhai na maisha endelevu ya mwananchi yoyote yule, iwe nyumbani, shuleni, mitaani ama mahali popote pale lazima usafi upewe kipaumbele ili kutunza uhai wetu.

Mbali na jitihada hizo  na wadau mbalimbali wa afya nchini, bado wapo baadhi ya watu katika jamii zetu wakiwemo viongozi ambao hawafurahishwi na juhudi hizi za kuweka mazingira katika hali ya usafi.

Watu hawa ama wanajua umuhimu wa suala hili kuwa ni jukumu la kila mtu, ama hawajui kwa maana kuwa wanatambua suala hilo ni la baadhi ya watu wachache na wao haliwahusu kabisa.

Watu hawa wako tayari kutoa kauli zilizo jaa fikra mgando zenye lengo la kukwamisha juhudi za kupambana na uchafu katika maeneo yetu tunayoishi.

Nasema haya kutokana na ukweli kuwa, wapo baadhi ya viongozi ambao kwao uchafu ni suala la kawaida na hawaoni kuwa lina madhara yake kama vile kusababisha vifo vya watu wanaowaongoza.

Ni hivi majuzi, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kalangalala mjini Geita, ambapo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Joseph Musukuma, alipotoa kauli ya kuzuia wananchi kufanya usafi.

Mwenyekiti huyu ambaye hupenda kujiita kuwa ni "Nape Nnauye wa Geita", anasema kuwa suala la usafi si kazi ya wananchi bali ya maofisa afya.

Sina hakika kama wakati akitoa maneno hayo alikuwa akimaanisha nini? Na wala lengo lake sikuweza kulibaini sawa na akaongeza kuwa hataki kusikia siku ya usafi iliyowekwa maalumu na Mkuu wa wilaya hiyo Manzie Mangochie ya kila siku ya alhamisi.

"Sitaki kusikia kabisa tena Mangochie day’ eti siku ya kufanya usafi, mimi kama mwenyekiti wa CCM Mkoa, napiga marufuku hiyo kazi ni ya mabwana afya si kazi yenu nyie wananchi" anasema Mwenyekiti huyu huku baadhi ya watu nao wakipiga kelele za kumshangilia.

"Mtu yoyote atakayekusumbua kisa eti umegoma kufanya usafi siku hiyo nipigie simu ili nipambane naye, hakuna kufunga duka kwa saa nne eti kufanya usafi wa eneo lako waachieni mabwana afya kwani tumewaajiri ni kazi yao hiyo si yenu," aliongeza.

Kauli kama hizi ni kauli zilizojaa mawazo mgando yasiyowatakia wananchi mema. Ni kauli zinazotolewa kama porojo zinazopaswa kutolewa na watu vijiweni na sidhani kama zinafaa kwa kiongozi kama huyu anayejifananisha na Nape kwa maana ya utendaji.

Hebu fikiria, ni kiongozi wa namna gani anayefikia hatua ya kupinga hata jambo jema kama hili la wananchi kufanya usafi katika maeneo yao? Ama anatoa kauli ilimradi apate makofi kwa watu wasio mtakia mema katika uongozi wake?.

Niseme tu ukweli kwamba kama ni ulevi wa madaraka, basi huenda Mwenyekiti huyu akawa amelewa mapema kuliko hata wenzie, na ndio sababu anatoa kauli za kilevi bila kujua kama zinasaidia kujenga chama chake ama ndizo zinazidi kukibomoa bila yeye kujua?.

Kila mtu mjini Geita, atakuwa shahidi kuwa, kabla ya kuanzishwa siku hii maalumu ya usafi, namna mji wa Geita ulivyokuwa ukinuka kutokana na kujaa uchafu kila mahali.

Ulikuwa hautamaniki kabisa jambo lililosababisha hata wafanyabiashara wa soko kuu la mji wa Geita kususia kulipa ushuru wa soko.

Kila mahali palikuwa ni uchafu, tena ni katika kipindi chake cha  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Geita, hali inayonishawishi kuwa huenda huyu ni mwenyekiti rafiki wa uchafu! Yawezekana na huku si kutafuta umaarufu tu kwa wananchi kwa kigezo cha kumwezesha kupata ubunge katika uchaguzi Mkuu ujao kama ambavyo amekwisha tangaza bali analo lake jambo ambalo limefichika.

Hivi, mheshimiwa Musukuma, hawa mabwana afya unaowasema wako wangapi katika mji huu wa Geita? Je kazi ya mabwana afya ni kufanya usafi na si kusimamia suala la usafi? Ama hawa mabwana afya hata kama tukiangalia majukumu yao wanayotakiwa kuyafanya kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira ndio hii ya kuzunguka mitaani na kwenye nyumba za watu na kuzoa uchafu?

Hizi ni porojo za kutafuta umaarufu ambazo hazina msaada  kwa wananchi bali zimelenga kuwaangamiza na magonjwa ya milipuko kama vile kuhara pamoja na kipundupindu na hakuna jambo jingine. Sidhani kama huo ubunge anaoutaka utamuongoza nani endapo watu wote watakuwa wamekufa kwa kukumbwa na magonjwa haya kutokana na kukithiri kwa uchafu katika maeneo yao.

Ameshindwa kubaini kuwa afya bora ni nguzo na rasilimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na
nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini

Musukuma pengine anashindwa kutenganisha masuala ya utendaji wa serikali na yale ya chama, amegeuka kiongozi wa porojo za kisiasa majukwaani na utendaji wa serikali sawia.

Mpango wa kufanya usafi si tu kwamba umeanzishwa hapa wilayani Geita pekee, bali ni sehemu nyingi zenye mpango kama huu  nchini na hata nje ya nchi na ni jukumu la kila mwananchi kushiriki katika suala hili.

Mojawapo wa mipango kama hii imewahi kutangazwa huko katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Mei 5, mwaka huu ambapo ilianzishwa siku maalumu ya "USAFI NI JUKUMU LETU".

Mpango huu utakuwa ukitekelezwa kila siku ya Jumamosi ya mwanzo wa mwezi na kuwa zitaanzisa kituo cha Bustani ya Forodhan saa 12 asubuhi, ambapo wananchi na wafanyabiashara wa taasisi za serikali na binafsi watashiriki kikamilifu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ni kwamba, suala la usafi ni jukumu la kila mtu, hivyo kila mtu anastahili kushiriki ili kudumisha usafi katika eneo lake analoishi na kuwa litasaidia kuyaweka mazingira ya mji wa Zanzibar na vitongoji vyake katika hali ya usafi endelevu.

Sasa kama hivi ndivyo huko Zanzibar na maeneo mengine, kwa nini Mwenyekiti huyu afikie hatua hii ya kulipinga jambo hili hapa wilayani Geita? Lengo lake nini? Watu waishi kwenye uchafu ili hatimaye waweze kufa na kubaki makaburi peke yake ama lengo lake nini hasa? Ama ana mpango wa kuanzisha au kuleta kampuni yake binafsi ya kuzoa uchafu ili ajipatie asilimia 10 ?.

Mwenyekiti huyu ameanza kuonesha kile kilichofanywa na madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita cha kumngoa kwenye nafasi ya umwenyekiti wa Halmashauri hiyo kuwa huenda kilikuwa sahihi wala hawakumuonea kama anavyowalaghai baadhi ya wananchi wasiomjua.

Hizi ni porojo tu ambazo katika kipindi hiki ambacho wananchi wengi wanajua kuchambua mazuri na mabaya haziwezi kusaidia bali zinazidi kumchambua na kumuonesha namna alivyo kiongozi wa kauli za kukurupuka bila hata kuyafanyia utafiti yale anayoyazungumza!

Hayati Julius Nyerere katika kitabu chake cha "Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania" aliwahi kusema kuwa nchi zetu hazitawaliwi na wanafalsafa wa Plato; watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala.

Anasema, wanasiasa wa namna hiyo, wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala, na wakisha kuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa.

Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere anasema, si busara kuwaachia wao wenyewe ndio wawe waamuzi wa lini waache kuwa watawala, hizi zote ni mbinu za viongozi wetu waheshimiwa kutaka kukiingiza chama katika njia moja tu nyembamba, na kutuburuza kama vipofu ili tuitumbukize nchi shimoni.

Kwa hakika hizi ndizo mbinu anazoziandaa Mwenyekiti huyu kwa kisingizo kuwa eti anakijenga Chama kwa kuwaita wenzie mafisadi na kuwa ni adui wa watu kumbe yeye mwenyewe ndie adui namba moja wa watu kwa kuwa anawazuia kufanya usafi ili wafe kwa magonjwa!




4 comments:

  1. hakika huyu si aina ya viongozi tunaowataka lakini ni aina ya viongozi tulionao,wanatafuta umaarufu hata katika kupinga maendeleo.CCM naomba msimwache hivihivi lazima m discipline hata kwa kukalishwa katika vikao halali au Sekretariet ya CCM Taifa impe maelekezo.Hayaiva kisiasa.

    ReplyDelete
  2. huko sahihi mwandishi na vema huyo msukuma akapata nakala hii ya gazeti akasoma akaona jinsi ulivyomchana na alivyo mweupe.Eti ndio viongozi wa ccm hawa ,shame on him

    ReplyDelete
  3. Sasa hivi viongozi wengi wanakibomoa chama badala ya kukijenga,

    ReplyDelete
  4. Tatizo shule, anadhani kusimamia masuala ya umma ni sawa na kuendesha kampuni ya mabasi! Aliivuruga Halmashauri ya Geita mpaka wakamtema, nashangaa kupewa tena wadhifa mkubwa hivyo.

    ReplyDelete