13 December 2012
Ustawi wa Jamii wajipanga kuwanufaisha wananchi wote
Na Mwandishi Maalum, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto imeeleza kuwa inaifanyia kazi Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ili kutekeleza lengo la kuwapatia huduma wananchi wote wanaostahili.
Sambamba na watoto wanaoishi katika mazingira magumu, watu wenye ulemavu, wasiojiweza pamoja na wale wanaoishi katika umaskini uliokithiri.
Hayo yalibainishwa juzi na uongozi wa wizara hiyo wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein katika kuangalia utekelezaji wa malengo makuu ya wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili-Juni 2011-2012 na Julai-Septemba 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahaya Mzee walishiriki kikamilifu.
Wizara hiyo ilieleza kuwa hatua hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro kadhaa katika sehemu za kazi nchini.
UTEKELEZAJI
Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa malengo makuu hayo ya wizara, Waziri wa wizara hiyo, Zainab Omar alisema sera hiyo itahusisha program mbalimbali za pensheni kwa wazee wote wakiwemo wakulima na wafanyakazi, afya kwa wazee na watoto, ulipaji wa fedha kwa familia zisizo na uwezo na kazi za malipo za kijamii.
Wizara hiyo ilieleza kuwa, kukamilika kwa sera hiyo kutasaidia sana kujenga ustawi wa jamii kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na utekelezaji wake.
Waziri Zainab, alieleza kuwa wizara imo mbioni kukamilisha Sera ya Jinsia ambayo kukamilika kwake kutasaidia sana kuelimisha jamii juu ya maana ya jinsia na umuhimu wake katika mazingira ya utekelezaji wa kazi pamoja na maisha ya kijamii.
WAZEE WANUFAISHWA
Alieleza kuwa, wazee wa Sebleni na Welezo wizara imeendelea kuwatunza na kuwahudumia vizuri kadri ya uwezo wao na tayari imeshaanzisha suala la kuwapatia milo mitatu kwa siku na kuendelea kuwapatia posho zao kama kawaida.
Pia, Wizara hiyo ilieleza jinsi ilivyolitafutia ufumbuzi suala la watoto wenye mazingira magumu nchini hasa kutokana na utafiti walioufanya huku ikieleza namna ilivyoendelea kuwa karibu na wanawake katika vikundi vyao vya kilimo, ujasiriamali, SACCOSS na Ushirika.
Pia ilieleza ilivyofanya utafiti wa awali juu ya uanzishwaji wa Benki ya Wanawake.
Wizara pia ilieleza haja ya upatikanaji wa mashine ya DN ili mapambano dhidi ya udhalilishaji yaweze kufanikiwa kwani ilieleza kuwa pamoja na juhudi zote zinazofanywa na wizara bado suala la udhalilishaji wa wanawake na watoto limeendelea kushika kasi.
WIZARA NYINGINE
Rais Shein pia alikutana na uongozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Kilimo na Malisili chini ya Waziri wake, Suleiman Othman Nyanga na kueleza nia ya wizara hiyo ya kutekeleza kwa vitendo katika kumkomboa mkulima wa Zanzibar kutoka katika kilimo duni kisicho na tija.
Wizara hiyo ilieleza kuwa imo katika kutekeleza dhima ya Mapinduzi ya Kilimo katika kuimarisha uchumi wa Taifa na kuondokana na umasikini.
Aidha, Wizara ya Kilimo na Maliasili ilieleza mikakati yake ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua ili yaweze kusaidia katika kilimo.
Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza jinsi ilivyopania katika suala zima la utafiti na kueleza jinsi ilivyoamua kuwashirikisha wakulima pamoja na washirika wengine sanjari na kuwashajiisha wakulima katika matumizi ya pembejeo na mbinu bora za kilimo.
Waziri Nyanga alieleza kuwa wizara hiyo imo katika mikakati ya kuwajengea uwezo wakulima katika kusarifu mazao ya wakulima pamoja na kuhifadhi kilimo na maliasili ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko.
Pia, Wizara imo katika juhudi za kupunguza uharibifu wa mimea na mazao utokanao na maradhi, wadudu, ndege na nzi na kueleza haja ya kuimarisha soko la ndani na kupunguza kusafirisha mazao nje ya nchi.
Sambamba na hayo, wizara hiyo ilieleza juhudi inazozichukua katika kuimarisha zao la Karafuu nchini.
RAIS SHEIN APONGEZA
Akitoa pongezi kwa nyakati tofauti alizokutana na wizara hizo, Dkt. Shein aliipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kwa juhudi zake inazozichukua katika kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Dkt. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati maalum ya kuimarisha sekta hiyo ili kuleta tija na mafanikio nchini huku akieleza azma ya serikali katika kuendelea kuwaunga mkono wakulima nchini.
*************
ANCHOR
Vijana waunda vikundi
kupambana na umasikini
Na Lilian Justice, Morogoro
VIJANA kutoka katika mikoa ya sita ya Tanzania Bara wameunda vikundi vya watu 30 kila mkoa kwa lengo la kutatua kero na kufikia malengo ya maendeleo katika mwaka 2030.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa niaba ya wenzao
vijana hao, Josina George kutoka Tanzania na Anders Nordeik kutoka Norway walisema kupitia Taasisi ya Kikristo inayoshughulika na masuala ya wanawake na vijana YWCA wameweza kupata nafasi ya kutembelea mikoa mbalimbali ili kutoa elimu ya kupunguza umaskini kwa vijana.
Walisema kuwa, lengo la kutoa elimu kwa vijana nchini ni kuwataka
kubadilika na kujua haki zao, kuwaondoa katika umaskini sambamba na
kujiona kuwa ni watetezi kwao na hata kwa wenzao.
Aidha, walieleza kuwa kupitia vikundi hivyo watatumia vipingamizi vilivyopo kama walivyofundishwa ambavyo havilingani kwa kila kundi kwani kila kundi la vijana lina vipingamizi vyake na kuweza kupunguza au kuzuia umaskini na kufikia malengo ya kumaliza umaskini huo ifikapo mwaka 2030 kama YWCA ilivyojiwekea.
Walivitaja baadhi ya vipingamizi ambavyo vijana walivitaja kuwa ni elimu ndogo, rushwa, utawala bora na sera mbovu zinazowakandamiza ambapo walisema wameamua kuangalia kundi la vijana kwani wanaamini kuwa ndio wenye nguvu na uwezo wa kubadilisha mambo ikiwemo
sera ambazo zinawakandamiza sambamba na kuwa viongozi wazuri wa
baadaye.
Hata hivyo walifafanua kuhusu malengo ya mpango wao huo kutakiwa uwe
umetekelezeka ifikapo 2030 na kusema kuwa wao wanaangalia Dunia
inavyokwenda kimaendeleo hawalingani na mipango mingi ya maendeleo ikiwemo ya kitaifa inayoishia 2015 na kutaka mipango endelevu inayoishia 2030 ambayo ndio wanayoifanya.
Vijana hao wametoka katika nchi za Misri, Urusi, Netherland, Norway, Sudan, Kenya na Tanzania kiongozi wao na kutembelea katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Dar es salaam.
********
3THIRD
Ofisa Mtendaji adaiwa
kutafuna fedha za umma
Na Mohamed Hamad Babati
JESHI la Polisi wilayani Babati Mkoa wa Manyara linamsaka Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Guse kwa tuhuma za kuvujisha fedha sh. milioni 11.3 ambazo zilichangwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari ziliyopo kijijini hapo.
Shule hizo zinazodaiwa kuliwa fedha zake ni Guse, Getabuske, Walahu zote zilizopo katika Kata ya Bashnet ambapo kwa pamoja wananchi walichanga kila kila kaya sh. 60,000 ili waondokane na adha ya kutumia gharama kubwa kulipa michango shule za jirani.
Kwa kujibu wa mmoja wa askari wa Babati ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini alidai wamepata taarifa za kutoroka kwa ofisa huyo kijiji hapo na kwamba jitihada za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea.
Alidai, wao kama jeshi la polisi kazi yao ni kulinda raia na mali zao hivyo kwa taarifa hiyo wako tayari kutumia gharama yoyote kupata mtuhumiwa ili aweze kufikisha mahakamani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Guse Kastuli Saxara alidai baada ya mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya Wilaya ya Bababati kukagua vitabu vya mahesabu vya mwaka 2011/2012 aligundua kuwepo kwa ubadhirifu huo ambapo alitoa taarifa kwa mwajiri wake.
“Baada ya mkaguzi kutoa taarifa kijijini, tukamwomba afikishe salamu hizo kwa Mkurugenzi mtendaji ambapo aliamwagiza Ofisa mtendaji wa Kata ya Bashnet, Julius Lawi kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji kufungua shtaka dhidi ya ofisa huyo,”alisema.
Naye Ofisa Mtendaji kata hiyo, Lawi alisema kuwa katika kata yake yameibuka malalamiko ya wananchi kuhusu viongozi kutuhumiwa kushindwa kutekeleza wajibu wao huku wengi wao wakihujumu miradi ya wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment