13 December 2012
SUMATRA komesheni upandaji nauli kiholela
SAKATA la mabasi yaendayo mikoani kupandisha nauli kila unapofika msimu wa sikukuu, si jambo geni kwa abiria ambao
huwa na kawaida ya kula sikukuu nje ya jiji la Dar es Salaam.
Siku zote tumezoea kusikia mamlaka husika zikiahidi kutoa adhabu kwa wamiliki wa mabasi ambayo yatabainika kutoza nauli kubwa lakini utekelezwaji wake bado hauna tija kwa abiria.
Kutokana na hali hiyo, wamiliki wa mabasi hayo hawana hofu yoyote ya kuchukuliwa hatua kama watapandisha nauli kiholela
na kukiuka bei elekezi wanayopaswa kutoza.
Mabasi mengi yanayotoka Dar es Salaam katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT), hutoza nauli kubwa kutokana na ongezeko la abiria.
Jambo la kushangaza, risiti zinazotolewa na watumishi wa mabasi hayo zimeandikwa kiwango halisi cha nauli tofauti na ile aliyolipa abiria ambaye hulazimika kufanya hivyo ili aweze kusafiri.
Inadaiwa kuwa, hali hiyo inatokana na kufidia hasara ambayo wamekuwa wakiipata kwenye kipindi chenye uhaba wa abiria.
Baadhi ya wafanyakazi wa mabasi hayo wanavuka mipaka zaidi na kulazimisha watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao wanasafiri na wazazi wao walipiwe nauli nusu ya ile anayolipa mzazi wake.
Sisi tunasema kuwa, umefika wakati wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), kuhakikisha vitendo vya kupandisha nauli kiholela katika kipindi hiki cha sikukuu vinakoma na wahusika wachukuliwe hatua ili iwe fundisho kwa wengine.
SUMATRA ishirikiane na makachero wa Jeshi la Polisi ili kuyabaini mabasi hayo kwani baadhi ya abiria, hutozwa nauli kubwa mara mbili ya ile anayopaswa kuilipa.
Baadhi ya wasafiri wenye kipato cha chini, hujikuta katika wakati mgumu zaidi hasa wanapofika kituoni na kukuta mabadiliko makubwa ya nauli tofauti na ile waliyoizoea siku zote.
Operesheni ya kukagua mabasi yanayopandisha nauli isiwe ya zima moto kutokana na ukubwa wa tatizo lenyewe hasa kwenye kipindi cha Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment