13 December 2012

Tusomeshe watoto tusiogope gharama


HIVI sasa, wazazi wengi mbali ya kufanya maandalizi ya sikukuu
ya Krismasi na mwaka mpya, wapo katika mchakato wa kuhakikisha watoto wao wanaandikishwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari. Wengine hulipia ada ili watoto wao waendelee na shule.

Ukweli ni kwamba, nchi nyingi zilizopiga hatua ya maendeleo, ziliona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ili wananchi wake waweze kutumia maarifa waliyonayo kutatua matatizo yao.

Serikali na wadau wa elimu nchini, wamefanya jitihada kubwa za kuboresha elimu kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).

Kimsingi jitihada hizo zimesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi walio shuleni, madarasa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia mbali ya changamoto zilizopo ambazo bado zinaendelea kutatuliwa.

Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuboresha mazingira ya elimu, ubora wa elimu haujafikia kiwango kinachotarajiwa kama inavyokusudiwa.

Ni jambo la kawaida kuona wahitimu wa darasa la saba hawajui kusoma wala kuandika. Uduni wa elimu kwa sasa unaendelea kushamiri ngazi zote kuanzia shule za msingi, sekondari v
yuo vya kawaida hadi vyuo vikuu.

Wanafunzi wanamaliza masomo na kutunukiwa vyeti wakiwa na maarifa finyu na uwezo mdogo wa kufikiri hivyo kushindwa kuchangia kikamilifu maendeleo ya jamii inayowazunguka.

Zipo sababu mbalimbali zinazochangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini moja wapo ni uhaba wa walimu katika shule za msingi, sekondari na vyuo.

Sisi tunasema kuwa, tatizo hili linachangiwa na walimu wetu kuzidiwa na mzigo wa wanafunzi darasani na mazingira duni
ya kufanyia kazi.

Hali hiyo inachangia walimu wengi kukata tamaa kwa sababu
ya kubinywa haki zao na kulipwa masilahi kidogo ambayo pia hawayapati kwa wakati.

Umefika wakati wa Serikali kutatua kero na kulipa stahiki mbalimbali za walimu ili wawe na moyo wa kufundisha.

Matarajio yetu ni kuona wazazi wanawajibika kuhakikisha watoto wao wanapelekwa shule kwa gharama yoyote ili waweze kupata maarifa ambayo ndio msingi wa maisha yao.

Tuwekeze kwenye elimu na kuboresha mafunzo kwa walimu wetu ili tuweze kufanikiwa. Bila walimu bora, hakuna elimu bora wala maendeleo.

No comments:

Post a Comment