18 December 2012

'Serikali waondoeni wavamizi Mto Ruaha'


Na Rehema Maigala

SHIRIKA la Huduma ya Habari Njema kwa Wote, limeishauri Serikali kuwaondoa wavamizi hasa wafugaji, wakulima wakubwa
na wadogo waliovamia mkondo na chanzo cha Mto Ruaha, uliopo Kilombero, mkoani Morogoro.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa shirika hilo, Askofu Charles Gadi, katika maombi maalumu ya kuombea mvua ambayo yamefanyika hivi karibuni katika mto huo kutokana na ukame unaendelea kuwaathiri wanyama baada ya mto kukauka.

Alisema kutokana na hali hiyo, makundi ya tembo na wanyama wengine wameanza kuvamia vijiji jirani ili kutafuta maji hivyo kusababisha wale migomba na ndizi za wananchi.

Aliongeza kuwa, Serikali iwajibike kuwaondoa wakulima na wafugaji ambao wamehamishia shughuli zao katika vyanzo vya
mto huo ili maji yaweze kutiririka katika Bwawa la Mtera.

“Mkulima anaweza kulima popote lakini wanyama hawana kwa kwenda hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha shughuli za kilimo
na ufugaji zinazofanywa na binadamu, zinasitishwa ili kuwanusuru wanyama hawa,” alisema Askofu Gadi.

Alisema shirika hilo limeamua kufanya maombi maalumu nchi nzima ili kuihamasisha jamii iwajibike kulinda mazingira pamoja
na mbuga mbalimbali za wanyama ikiwemo Ruaha.

Mkuu wa Hifadhi ya Wanyama Ruaha, Bw. Stephano Qolli, alisema ukame uliotokea katika mto huo umechangiwa na shughuli za kilimo zinazofanywa kandokando ya mto na vyanzo vyake vilivyopo katika milima ya Mpanda, Kipengele na Usangu.

Alisema kutokana na tatizo hilo, baadhi ya wanyama ambao huishi kwa kutegemea maji kama viboko, tayari wameanza kugama katika hifadhi hiyo pamoja na wanyama wengine.

“Maji yakokosekana katik mto huu ni hatari sana, wanyama wengi huambukizana magonjwa kama kimeta, wengine wanaliwa na wanyama wakali kama Simba na Chui wanapogania maji
machache yaliyopo mtoni,” alisema.

Aliiomba Serikali kuhakikisha chanzo cha mto huo kinatunzwa
ili wanyama waliopo wasiweze kutoweka.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa kitongoji cha Ofisini, Kijiji cha Tungamalenga, Wilaya ya Iringa Vijijini ambacho kimepakana na mbuga hiyo, Bw. Greyson Ngwale, alisema amekuwa akiona makundi ya tembo na wanyama wengine wakiingia kijijini hapo kutafuta maji na vyakula.

Novemba mwaaka huu, shirika hilo lilifanya maombi kama hayo katika mikoa ya Katavi na Kilimanjaro kabla ya kwenda mkoani Iringa kwenye Hifadhi ya Ruaha.

No comments:

Post a Comment