18 December 2012

NHC lafanikiwa kukusanya bil. 5/-


Na Goodluck Hongo

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limeongeza makusanyo yake kutoka sh. bilioni 2.6 hadi 5.75 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Kesogukewele Msita, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki na kuongeza kuwa, mafanikio hayo yametokana na usimamizi
mzuri wa ukusanyaji mapato ya shirika.

Alisema awali baadhi ya watu walilifanya shirika hilo  shamba la bibi ambapo hivi sasa wamepata ardhi ekari 28,000 za akiba.

Aliongezza kuwa, mafanikio mengine ni kuboreshwa kwa masilahi ya wafanyakazi hivyo kuongeza uwajibikaji pamoja na kuzishawishi benki mbalimbali nchini kuwakopesha wanunuzi wa nyumba baada ya mabadiliko ya Sheria ya Mikopo.

“Wakati shirika hili linafanya mabadiliko, tulipata shida kubwa kwani ilionekana tunazuia masilahi ya baadhi ya watu ambao walilifanya shirika kama kitega uchumi chao kinyume cha
sheria na utaratibu,” alisema Mhandisi Msita.

Aliongeza kuwa, upandishaji kodi kwenye nyumba za shirika umekuwa ukizingatia uwezo wa wananchi ambapo ambapo hadi
sasa, kodi za nyumba hazijafikia asilimia 60 ya soko lakini lengo
la shirika ni kufikisha asilimia 85 ifikapo mwaka 2015.

Aliziomba halmashuri zote nchini na Serikali, kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili liweze kutekeleza malengo yake ya kuwawezesha wananchi kupata nyumba.

No comments:

Post a Comment