18 December 2012

Katiba Mpya ikomeshe uzembe kwa watendaji



KATIBA ni mfuko wa kanuni ambazo zinaongoza dola na kutoa mwongozo wa taratibu za mfumo wa Taifa kujitawala kwa mujibu wa kanuni na sheria ili kubaini wajibu na haki kwa watawala na watawaliwa.


Historia ya mwanadamu amepitia mifumo mitano ya uhusiano katika uzalishaji mali. Kati ya hiyo, mitatu ni tabaka tawala na tawaliwa isipokuwa mfumo wa kijima na kijamaa.

Hakuna Mtanzania aliyejitenga katika mifumo hii ambayo ndiyo chimbuko la katiba. Baada ya shughuli za binadamu kuongezeka ili kujikwamua na unyonge katika mazingira anayoishi, ndipo likaingia suala la ubinafsi wa kujimilikisha njia kuu za uzalishaji mali.

Hali hiyo ilichangia ukandamizaji, unyonyaji na ufedheheshaji wanyonge ambao walinyimwa haki kwa misingi ya kibaguzi.

Tatizo hilo lilichangia uzalishaji mali kuwa wa kitabaka, ongezeko la migogoro ya haki, usawa na kugawana ziada iliyopatikana katika uzalishaji.

Migogoro hiyo ilifanikiwa kuangusha mifumo kandamizi lakini bado uhusiano wa kitabaka, uliendelea kuwepo kwa sababu kilichobaki ni taratibu za kisiasa kufanya upendeleo kwa walio mstari wa mbele kuwaingiza katika kundi lenye masilahi na tabaka tawala.

Jamii kubwa, imekosa haki ya kutumia rasilimali za nchi ambazo wamepewa na Mungu kwa tamaa na ubinafsi. Hiki ndicho kitatokea kwa kizazi cha sasa ambacho kinadai Katiba Mpya.

Angalizo ni kwamba, kama katiba itaandikwa haitajadiliwa kwa kina na wananchi wote ili sera na hoja ziweze kueleweka, wananchi watakuwa na uamuzi wa woga, hivyo kufungua kitanzi cha umaskini, ujinga na maradhi.

Changamoto hizo zitakoma kama kanuni za Katiba Mpya, zitalinda rasilimali za Taifa kwa masilahi ya Watanzania wote. Katiba kama mfumo wa kanuni za kutetea haki na wajibu, lazima izingatie maoni ya wananchi badala ya kutetea masilahi ya tabaka tawala.

Katiba Mpya inapaswa kukomesha umaskini, ujinga na maradhi badala ya kuwalinda wanasiasa na viongozi walio madarakani ili kuharakisha maendeleo.

Sisi tunasema kuwa, Tanzania ina rasilimali nyingi za kuweza kuhudumia wananchi wake. Taifa lenye vipaumbele vya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na teknolojia, mafanikio yake yatatokana na sheria imara ambayo ni katiba.

Katiba Mpya iwawajibishe watendaji wa Serikali na wananchi wanaotumia rasilimali za nchi kujinufaisha na izingatie demokrasia kwa watu wenye mapenzi mema kwa faida ya Taifa lao.

Kwa mfano, watoto wetu huandaliwa kitaaluma na wasomi ambao baadhi yao, hawana mwamko wa kumuandaa mwanafunzi ili afaulu mitihani hivyo matokeo yake ni kuandaa wataalamu dhaifu.

Tungependa kuona Katiba Mpya inakomesha uzembe katika utendaji kazi wa shughuli za maendeleo kwani Tanzania ni nchi yenye neema lakini wananchi wananung'unika kutokana na ugumu wa maisha.

Imani yetu ni kwamba, wananchi wana nguvu ya kuzalisha mali ila bado wanateseka kwa sababu ya kukosa katiba yenye usawa na haki.

No comments:

Post a Comment